Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Primary Question
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: - Je, lini Serikali itaweka utaratibu wa mbolea kuwekwa kwenye vifungashio vya kilo tano, kumi, 15, 25 na 50?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na nipende kuishukuru sana Serikali kwa maelekezo ambayo imeshayatoa mpaka sasa hivi. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; tutarajie lini sasa hizi mbolea zilizofungashwa kwenye kilo 5, 10, 20 na 50 zitafika hasa madukani na kwa mawakala ili wananchi waweze kufaidika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; bei elekezi imekuwa inagusa zaidi mfuko wa kilo 50 wa mbolea; je, ni lini Serikali itatoa bei elekezi kwa kilo moja ya mbolea?
Name
Hussein Mohamed Bashe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nzega Mjini
Answer
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kakunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lini mbolea hizi zitaanza kuonekana? Nataka tu nimtaarifu kwamba mbolea hizi tayari zimeshaanza kufungwa na Mkoa wa Tabora kwenye ghala kuu la Yara ni moja kati ya ghala ambalo linafunga mbolea hizi za kilo tano na hivi karibuni lilipata tatizo baada ya kugundua kwamba tulivyowapa nafasi ya kufunga mbolea za kilo tano/tano waliamua kufungasha vilevile na mbolea ambazo zimepitwa na wakati, tukalifunga ghala la Tabora na ghala la Iringa kwa sababu hiyo lakini makampuni tayari yameshaanza kufunga na kuuza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lini zitaanza kuuzwa kwa bei elekezi? Bei elekezi ya kilo 50 kama ni shilingi 75,000 maana yake mfungashaji yoyote anapofungasha kilo tano hatakiwi zile kilo tano/tano mifuko 10 thamani yake izidi kiwango cha shilingi 75,000 ya bei elekezi na tumeshachukua hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichukua hatua kwa kampuni kwa Kampuni ya Minjingu tuliwagundua kwamba wanachukua mfuko wa kilo 50 wanafunga kilo tano/tano wanauza shilingi 13,000 maana yake ukijumlisha mifuko kumi ya kilo tano/tano inakuwa 130,000 tukawachukulia hatua na natumia Bunge lako Tukufu kuwaambia makampuni yote wasibadili msingi wa bei elekezi kama mbolea ni shilingi 75,000 kilo 50, maana yake ukifunga kilo 20 ni lazima thamani ya kilo 20 isizidi cost per unit ya kilo 50.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, natumia nafasi hii kuwaambia TFRA popote walipo wahakikishe wanafatilia ili wafanyabiashara wasi-take advantage katika jambo hili. Mwongozo wa bei utakaotangazwa hivi karibuni namwagiza Mkurugenzi wa TFRA kwamba tumekuwa na utaratibu wa kutoa bei elekezi ya kilo 50 sasa waweke na ujazo wa kilo tano, 10, 20 na 50. (Makofi)
Name
Selemani Moshi Kakoso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Vijijini
Primary Question
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: - Je, lini Serikali itaweka utaratibu wa mbolea kuwekwa kwenye vifungashio vya kilo tano, kumi, 15, 25 na 50?
Supplementary Question 2
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Niipongeze Serikali kwa kuleta ruzuku ya pembejeo. Wakulima wa zao la tumbaku mwaka jana hawakunufaika na ruzuku iliyotolewa na Serikali. Naomba kujua kwa msimu huu wa kilimo Serikali imejipangaje kuwapa ruzuku wakulima wa zao la Tumbaku?
Name
Hussein Mohamed Bashe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nzega Mjini
Answer
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kakoso na wakulima wote wa tumbaku. Serikali inafanya mkokotoo wa namna gani wakulima wa tumbaku na wenyewe waweze kupata kuwa sehemu ya skimu ya ruzuku na tutatoa mawasiliano kupitia muunganiko wao wa TCJE ili waweze kuelewa namna gani na wao watafaidika katika msimu huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana na mwaka huu wakulima wa tumbaku hatukuwaingiza kwenye mfumo wa ruzuku kwa sababu mfumo wetu wa ruzuku ulitazama zaidi mazao ya chakula kuliko mazao ambayo sio ya chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tunatoa ruzuku kwenye pamba, tunatoa ruzuku kwenye korosho hatutoacha kuwapa ruzuku wakulima wa tumbaku kama wakulima wengine katika nchi yetu. (Makofi)
Name
Luhaga Joelson Mpina
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisesa
Primary Question
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: - Je, lini Serikali itaweka utaratibu wa mbolea kuwekwa kwenye vifungashio vya kilo tano, kumi, 15, 25 na 50?
Supplementary Question 3
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa usambazaji na ugawaji wa mbolea katika msimu wa kilimo 2022/2023 uligubikwa na changamoto nyingi ikiwemo wakulima kuuziwa mbolea feki, mbolea nyingi kutoroshwa lakini wakulima wengi kupelea mbolea na kusababisha hasara kubwa.
Je, katika msimu huu wa kilimo 2023/2024 Serikali imejipanga vipi kutatua changamoto zilizojitokeza mwaka jana na kuleta hasara kubwa kwa wakulima?
Name
Hussein Mohamed Bashe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nzega Mjini
Answer
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Luhaga Mpina, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba tulivyoanza mfumo wa ruzuku kulikuwa na changamoto. Changamoto zilikuwa nyingi, tulikuwa na changamoto ya mfumo wa distribution lakini vilevile changamoto ya waagizaji wa mbolea kuamini kuwa Serikali itawalipa, changamoto ya watu kutokuwa waaminifu. Nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote, mkifanya tathimini ya mwaka jana na mwaka huu changamoto zilizokuwepo mwaka jana nyingi zimetatuliwa na Serikali na tutaendelea kuboresha mfumo wa ruzuku kila siku kwa sababu changamoto zinajitokeza mpya kila kukicha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwaka huu tumekumbana na changamoto ya baadhi ya wafanyabiashara kwenda kuanza kutafuta njia ya kutorosha mbolea. Kwa sababu wameshindwa kuiba ndani ya mfumo, wameshindwa kuingiza takwimu hewa, sasa wameanza kutaka kutorosha katika boarder, Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Kigoma imetusumbua sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nilitaarifu Bunge lako tumewakamata wafanyabiashara ambao walikuwa wanataka kutorosha mbolea kwa njia ya barabara na sasa hivi wamepandishwa Mahakamani kwa makosa ya uhujumu uchumi. Niendelee kuwaambia Watanzania na wakulima kwamba Serikali itaendelea kuboresha mfumo, hatutouacha mfumo wa ruzuku kwa sababu tunaamini kwamba tuna wajibu wa kuwasaidia wakulima wadogo na tutaendelea kukabiliana na changamoto zinazojitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hauwezi kufananisha changamoto za mwaka jana na mwaka huu. Mwaka huu hakuna changamoto ya usambazaji, tumeusisha vyama vya ushirika, tumeusisha halmashauri husika katika usambazaji wa mbolea, tumeendelea kuujenga mfumo kwa kutumia wenzetu wa eGA kuongeza security kwenye mfumo wetu ili kupunguza matatizo yaliyokuwepo mwaka jana. Kwa hiyo naamini kwamba tutaendelea kuuboresha mfumo wetu siku zinavyozidi kwenda. (Makofi)
Name
Kunti Yusuph Majala
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: - Je, lini Serikali itaweka utaratibu wa mbolea kuwekwa kwenye vifungashio vya kilo tano, kumi, 15, 25 na 50?
Supplementary Question 4
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na mimi kunipatia nafasi nimuulize Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza. Kwenye majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kuna Kampuni tatu ambazo Serikali ilishatoa maelekezo kwa ajili ya kufungasha mbolea kwenye kilo tano, kumi na kadhalika; lakini mpaka sasa ni Kampuni moja tu ambayo ndiyo imeanza kufunga mbolea kwa hivyo vifungashio vidogo vidogo. Nayo imeenda kufungasha na imefanya hujuma, imeweka na mbolea ambayo haistahili, wamefunga. Nini kauli ya Serikali kwa Makampuni haya ambayo tayari Serikali imetoa maelekezo kufungasha mbolea kwenye vifungasho vidogo vidogo wasipotekeleza hili kwa wakati ili wakulima wetu waweze kupata mbolea na iweze kutumika kwa kuleta tija kwa wakulima wetu?
Name
Hussein Mohamed Bashe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nzega Mjini
Answer
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani labda wakati najibu Mheshimiwa Mbunge hakunielewa vizuri. Nimesema Kampuni tatu zimeishaanza kufungasha, tatu, ambazo ni ETG, YARA na Minjingu kati ya hizi tatu ni moja ndiyo tumeikuta na tatizo katika mikoa miwili; Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Iringa, na tunaendelea kuzihamasisha kampuni zote ziendelee kufungasha katika ujazo mdogo mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukafahamu kwamba segment inayotumia mbolea kilo moja na segment inayotumia mbolea kilo tano ni wakulima wadogo, wadogo wa bustani ambao si sehemu kubwa na tujue kwamba hii ni biashara. Kwa hiyo tutaendelea kuwahamasisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile Wizara sasa hivi tumeiwezesha TFC ili TFC Kampuni ya Serikali ifanye kazi kubwa ambayo kampuni binafsi hazioni maslahi makubwa katika eneo hilo na TFC hivi karibuni na yenyewe itaanza kufungasha katika vifungashio vidogo vidogo ili wakulima waendelee kupata huduma wanayotaka. (Makofi)