Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Simai Hassan Sadiki

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nungwi

Primary Question

MHE. SIMAI HASSAN SADIKI aliuliza: - Je, sababu zipi zinasababisha eneo linaloathiriwa na mabadiliko ya tabianchi kupewa kipaumbele cha utekelezaji wa Mradi ili kunusuru hali hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuwa mara nyingi nimekuwa nikisimama Bungeni hapa na kutaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kuwaathiri kule Nungwi lakini majibu yamekuwa yakitofautiana katika swali moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanataka kujua je, eneo lile unalolizungumzia hapa kwamba bado halijakidhi vigezo na masharti vilivyowekwa ili kuweza kupewa kipaumbele?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa tafiti nyingi zimeshafanyika katika kubaini athari za mabadiliko ya tabianchi kule maeneo ya Nungwi katika maeneo ya jamii na maeneo ya fukwe.

Je, Serikali kupitia Wizara yako ina mkakati gani au inawahakikishiaje wananchi kutengewa fedha katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika eneo lile?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, najibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Simai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie fursa hii nimpongeza Mheshimiwa Simai kwa kazi nzuri anayoifanya hasa kutokana na athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi na jinsi ambavyo anawasaidia na kuwasemea wananchi wake kwenye Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo ambalo linatakiwa lijengwe ukuta kwa upande wa Nungwi limekidhi vigezo na lina kila sababu ya kufanya hivyo na ndio maana tumeanza kufanya utafitii na ndio maana viongozi wa SMZ na SMT wameshafika pale na ndio maana tumeshaliombea bajeti kwa ajili ya kulifanyia kazi kwa sababu tumeona athari ya kwamba pale pana kila sababu ya kusaidiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu Msheshimiwa Simai kwamba kutokana na vigezo hivyo tulivyovitaja eneo lile lina kila sababu ya kushughulikiwa na kusaidiwa na kufanyiwa kazi kama ambavyo Serikali imeliahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwahakikishie wananchi wa Jimbo la Nungwi niwaambie kwamba athari ya kuingia maji ya chumvi kwenye mitaa ama kwenye makazi ya wananchi hili jambo niwaambie linaenda kuondoka na ukuta ambao wanaulalamikia unakwenda kujengwa. Kwa nini utajengwa? Kwa sababu kwanza Serikali imeguswa na jambo lile lakini utakwenda kujengwa kwa sababu tayari tumeshaanza kujenga kuta kama hizi, tumejenga kule Pemba, Sepwese na tumeanza kujenga kule Mtwara Mikindani maana yake na Nungwi tunakwenda kujenga ukuta huu, nashukuru. (Makofi)

Name

Khalifa Mohammed Issa

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Mtambwe

Primary Question

MHE. SIMAI HASSAN SADIKI aliuliza: - Je, sababu zipi zinasababisha eneo linaloathiriwa na mabadiliko ya tabianchi kupewa kipaumbele cha utekelezaji wa Mradi ili kunusuru hali hiyo?

Supplementary Question 2

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba niulize swali moja. Mtambwe Mkuu ni kisiwa cha historia ambacho kwa kiwango kikubwa kimevamiwa na maji ya chumvi kiasi ambacho wananchi wanahama. Je, na hichi hakijapata kipaumbele cha kuonekana ipo haja ya kushughulikiwa?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, moja miongoni mwa kazi kubwa ambayo tumeamua sasa tuanze kuifanya ni kuhakikisha kwamba tunarejesha mazingira yaliyoharibika kutokana na maji ya chumvi kwenye maeneo ya visiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya miongoni mwa maeneo ambayo tumeshataka kuyapa kipaumbele ni eneo la hichi Kisiwa cha Mtambwe Mkuu. Kubwa tu nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba na yeye aendelee kutusaidia kusema na wananchi. Shughuli hizo zinazoendelea za kibinadamu zisiendelee kuliathiri visiwa vyetu, shughuli za utalii, shughuli za uvuvi, shughuli nyingine za ulimaji wa mwani zione namna ambavyo zinatunzwa na kuhifadhi mazingira haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kisiwa cha Mtambwe Mkuu tunakwenda kurekebisha ili kuondosha athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi, nashukuru.