Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Primary Question

MHE. DEODATAUS P. MWANYIKA aliuliza: - Je, kwa nini Sheria za Ardhi zinazokusudiwa kutumika kwenye miji zinatumika maeneo ya vijijini?

Supplementary Question 1

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mheshimiwa Waziri, nakushukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo, uhalisia uliopo ni kwamba, kuna mkanganyiko mkubwa sana kwenye halmashauri za miji ambazo zina vijiji. Sasa, Waziri atakubaliana nami kwamba, ni wakati sasa wa kutoa maelekezo kwa sababu sheria inataka utayari wa eneo kabla halijawa declared planning area. Maeneo mengi yamekwenda kuwa declared planning area kabla hayajawa tayari na ni maeneo ya vijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa yuko tayari kutoa maelekezo ili kufanyike marekebisho ya kutangaza upya maeneo ya vijiji yasitawaliwe na Sheria za Miji? Ahsante.

Name

Jerry William Silaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukonga

Answer

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Deodatus Mwanyika, kwa kuendelea kufuatilia maslahi ya wananchi wake wa Jimbo la Njombe Mjini. Ni kweli Sheria ya Mipango Miji, Sura ya 355 kifungu cha 77(1)(b) kinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya Ardhi, kutoa Kanuni zinazoongoza upangaji wa miji (Planning Space Standard). Vilevile mwaka 2018 Kanuni hiyo ilitolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilithibitishie Bunge lako kwamba Kanuni hii tumeisimamisha na tumetoa maelekezo kwa wataalam wa ardhi wa Wizara ya Ardhi, kuipitia upya na kutoa Kanuni ambayo itaendana na hali halisi ya maeneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni hii ndiyo inayohusika kwenye ujenzi wa vituo vya mafuta vile vyenye ardhi ndogo, inahusika kwenye mashamba ya mijini ya ekari tatu na ukiangalia hali halisi ya Mji wa Njombe kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni mji wa kilimo. Pia kilimo kinacholimwa pale ni kilimo cha parachichi na sisi Wizara ya Ardhi hatuwezi kuwa kikwazo cha kuendeleza zao la parachichi ambalo linalimwa kwenye Wilaya ya Njombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kuirejea Kanuni hiyo na tutamshirikisha Mheshimiwa Mbunge wa Njombe na Wabunge wengine wenye maeneo ya vijiji ambayo na sura ya kijiji, ili Kanuni itakayotoka iweze kuendana na mazingira ya wananchi hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.