Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Frank George Mwakajoka
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Tunduma
Primary Question
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatumia wataalam wake katika kupanga Miji na kuondokana na ujenzi holela unaoendelea nchi nzima?
Supplementary Question 1
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ili niweze kuuliza swali la nyongeza kwa niaba ya wananchi wangu wa Mji wa Tunduma. Swali la kwanza; Mji wa Tunduma ni mji uliopo mpakani mwa Tanzania na Zambia na ni lango kuu la nchi za Kusini na Kati mwa Afrika. Kwa tafsiri hiyo ni kwamba wageni wote kabla hawajingia katika nchi ya Tanzania ni lazima wapitie Tunduma kutoka katika nchi hizo.
Je, Serikali ina mpango gani wa makusudi na wa haraka wa kupima ardhi katika Mji wa Tunduma ili kuondoa ujenzi holela unaoendelea kwa hivi sasa? (Makofi)
Swali la pili; nini mwongozo wa Wizara ya Ardhi ikishirikiana na TAMISEMI kupitia Halmashauri zetu kwenye Idara ya Ardhi ili kutoa fursa kwa Halmashauri kukopa fedha katika taasisi za fedha, lakini pia kukubali makampuni binafsi ambayo yanaweza yakapima ardhi mfano UTT katika maeneo yetu ili kuhakikisha kwamba tunapunguza ujenzi holela katika maeneo yetu ya Mji wa Tunduma na maeneo yote nchini? (Makofi)
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza, nikubaliane naye kwamba ni kweli Tunduma ni lango kuu na lipo mpakani na uingiaji wa watu pale ni mkubwa sana kwa hiyo panahitaji kuwa na mipango iliyo thabiti. Ameuliza tuna mpango gani wa kupima ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, jukumu la kupima ardhi siyo la Wizara peke yake, Halmashauri zenyewe zinatakiwa kuwa na mipango yake ambayo inakuwa imeandaliwa. Wizara inakwenda kutoa msaada hasa wa wapimaji labda na vifaa kupitia Kanda pale ambapo Halmashauri imeshindwa yenyewe kutekeleza jukumu hilo. Kama mna mpango huo tayari Tunduma, Wizara yangu itakuwa tayari kushirikiana nanyi kuhakikisha kwamba maeneo yale yanapimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ametaka kujua nini mwongozo wa Wizara katika suala zima la upimaji kwa kutumia mashirika au makampuni binafsi ukatolea mfano wa UTT. Naomba niseme tu kwamba, Wizara tayari imeshabainisha makampuni 55 na orodha kamili tunayo na Wabunge kama mtahitaji tutawatolea copy tuwape ili muweze kushirikiana nayo kwa sababu baadhi ya makampuni mengine siyo wakweli katika kufanya kazi, lakini tunayo ambayo tumeainisha yapo makampuni 55 ambayo tumeruhusu yanaweza kufanya kazi na Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa ni ninyi wenyewe Waheshimiwa kuzungumza na yale makampuni na kuweza kukubaliana namna bora ya kuweza kufanya upimaji. Kwa sababu wakati mwingine yale makampuni yanaweza yakapima kwa kutumia rasilimali zao, lakini kuna namna ambavyo Halmashauri inakubaliana nao wawalipe kiasi gani katika kazi wanayofanya au wanaweza wakawasiliana na wananchi moja kwa moja wenye mashamba makubwa, lakini kupitia Halmashauri kujua mpango wenu ukoje katika maeneo yale, wanakubaliana namna ya kulipana katika zoezi hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, milango iko wazi, mashirika na makampuni mbalimbali yapo, yanaweza yakafanya kazi hiyo ni kiasi cha Waheshimiwa kufanya mawasiliano nayo. Orodha ipo kwa yeyote atakayehitaji tutatoa copy ili aweze kujua ni kampuni gani anaweza akafanya nayo kazi. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved