Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Josephat Mathias Gwajima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kawe

Primary Question

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: - Je, ni nini Mpango wa Serikali kudhibiti Mto Nakasangwe na Mto Tegeta na kadhalika inayopanuka kwa kasi na kutishia maisha ya watu na mali katika Jimbo la Kawe?

Supplementary Question 1

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya mvua nyingi zinazoendelea katika Jiji la Dar es Salaam mito mingi imejaa na kumwaga maji kwenye nyumba za wananchi; na watoto wengi wameshindwa kwenda shule kwa sababu ya mito hiyo na imehatarisha maisha ya watu na nyumba za watu.

Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kusaidia kudhibiti mito hii isiharibu maisha ya watu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Mto Nakasangwe, Mto Tegeta, Mto Mbezi, Mto Ndumbwi na Mto Mpiji miaka miwili iliyopita ilikuwa na upana wa mita 50 tu leo ina upana wa mita 100.

Je, Waziri utakubali kwenda pamoja na mimi ukaione mito hii wewe mwenyewe na utafute ufumbuzi wa kudumu wa kudhibiti mito hii kwa ajili ya kuokoa mazingira? (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge Askofu Gwajima kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua fursa hii kumpa pole sana Mheshimiwa Gwajima kwa kuingiliwa kwa maji katika maeneo yale, mito mingi imefurika. Lakini pia nachukua fursa hii kumpongeza sana mpaka jana usiku nilikuwa naangalia kwenye vyombo vya habari yupo Kawe anawasaidia Wananchi, anashirikiana nao katika janga hili la kuingiliwa kwa maji. Nataka kuchukua fursa hii pia kuwapa pole Watanzania wote ambao wameathirika na mvua kwa njia moja au nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa mipango ya dharura ambayo tunakwenda kuifanya kama Serikali kuhakikisha kwamba tunatatua hii changamoto ya kufurika kwa mito na maziwa na maeneo mengine ambayo yanajaa maji yanaathiri wananchi; kwanza ni kwenda kutafuta fedha kuhakikisha kwamba tunajenga kuta ambazo zitazuia maji yasiingie kwenye makazi ya wananchi. Pili tutahakikisha tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wajue athari za mvua na athari za kukaa kwenye mabonde, na pia wajue namna ya kuweza kuondoka mapema kabla mvua hizi hazijaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti vilevile, tunakwenda kuishirikisha jamii kwenye masuala ya usafi wa mito, mitaro na maeneo mengine ambayo yanakwamisha maji yasiende mwisho wa siku yanasabisha maafa. Kubwa ni utekelezaji wa Sheria ile ya mita 60 kama ilivyozungumzwa katika Kanuni ile ya 191 ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa jambo hili na kazi kubwa anayoifanya Dkt. Gwajima nipo tayari kwenda Jimboni Kawe kushirikiana na Wananchi kuhakikisha kwamba tunawasaidia katika kuondokana na hii changamoto ya uingiaji wa maji katika makazi yao, nakushukuru. (Makofi)

Name

Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Primary Question

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: - Je, ni nini Mpango wa Serikali kudhibiti Mto Nakasangwe na Mto Tegeta na kadhalika inayopanuka kwa kasi na kutishia maisha ya watu na mali katika Jimbo la Kawe?

Supplementary Question 2

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuunga mkono kabisa Dkt. Gwajima mchungaji, ameelezea vizuri. Mimi nina video moja hapa ambayo ukimaliza kujibu maswali tuonane. Hali ni mbaya Tegeta na kuna chanzo chake, ni kwa sababu walipokuwa wanajenga barabara ile ya kwenda Bagamoyo waliziba mifereji. Hali ni mbaya ukirudi hapa Mheshimiwa niruhusu nikuonyeshe video ya hali mbaya iliyoko. Nakupongeza Mheshimiwa kwa kazi uliyofanya hali ni…

MWENYEKITI: Swali?

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali kupitia TANROADS watazibua mifereji waliyoziba walipokuwa wanajenga barabara ya kwenda Bagamoyo? Hali ni mbaya naomba nimuonyeshe na video. (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wakati mwingine Serikali inapokuwa inafanya utengenezaji au ukarabati wa miundombinu hasa ya barabara zipo changamoto ndogondogo huwa zinatokea. Siku zote tunapojenga lazima tutabomoa, na tukibomoa lazima kuna kasoro zitajitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuambia Mheshimiwa Mama Sitta kwamba tuko tayari kushirikiana na Wizara inayohusika kwa maana kwamba Wizara nyingine za kisekta. Lengo na madhumuni ni wanapojenga au wanaporekebisha miundombinu ya barabara wahakikishe kwamba wanatengeneza mazingira mazuri ya kupitisha maji ili kipindi cha mvua nyingi maji yaweze kupenya na yaende baharini yasiathiri makazi ya watu, nakushukuru. (Makofi)

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Natumia nafasi hii kuwaelekeza Meneja wa Mikoa TANROADS kote nchini kwenda kwenye maeneo ambayo yana changamoto kama Waheshimiwa Wabunge walivyosema na kuleta haraka iwezekenavyo namna ambavyo tunaweza tukakabiliana na jambo hili kwa dharura, ahsante sana. (Makofi)