Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Najma Murtaza Giga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: - Je, lini Serikali itarudisha masomo ya kazi za mikono kama useremala, mapishi, kushona, kilimo, ujenzi kwa shule za Msingi na Sekondari?

Supplementary Question 1

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nitumie fursa hii kuipongeza sana Serikali kupitia Wizara ya Elimu, kwa kuendelea kuboresha sekta ya elimu nchini, hususan katika masuala ya kazi ya masomo ya kazi za mikono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la nyongeza ni moja tu. Kwa vile Baraza la Taifa la Mitihani pamoja na Elimu ya Juu ni masuala ya Muungano au ni mambo ya Muungano, na kwa madhumini ya kuwajengea msingi wa aina moja, vijana wetu wote wa Kitanzania. Je, Serikali ya Muungano kupitia Wizara ya Elimu inashirikiana vipi na Wizara ya Elimu Zanzibar ili kuhakikisha kwamba misingi yao ya elimu inakuwa ya aina moja na waweze kufanya mitihani ya aina moja? Ahsante sana.

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Giga Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba wakati wa uandaaji wa mitaala hii, uratibu ulifanyika kwa kutumia taasisi zetu zote mbili ile Taasisi ya Elimu Zanzibar pamoja na Taasisi ya Elimu ya Tanzania Bara. Vilevile Wajumbe wa Kamati waliohusika katika marekebisho ya mitaala hii walitoka katika pande zote mbili za Muungano, kwa maana ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile maoni juu ya mtaala huu yalipokelewa katika pande zote mbili za Muungano. Tulifanya makongamano pamoja na mikutano kule Zanzibar, vilevile tulifanya makongamano na mikutano mbalimbali huku Tanzania Bara. Kwa hiyo, nimuondoe wasiwasi hili limezingatiwa kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tuliweza kuwasilisha rasimu hii ya mitaala kwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kabla ya mitaala hii haijaenda kwenye ithibati nyingine. Nimwondoe wasiwasi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tutaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania Bara katika kuhakikisha kwamba mitaala hii inatekelezwa na wenzetu vilevile wa Zanzibar nao vilevile wafanye mapitio ya mitaala yao, ndiyo itakayokwenda kutekelezwa na tutakuwa sasa tunakwenda pamoja. Nakushukuru sana.