Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. David Mathayo David
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Same Magharibi
Primary Question
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:- Je, lini Kata za Ruvu, Msindo, Mshewa, Vudee, Mhezi, Tae na Suji - Same zitapelekewa mawasiliano ya simu?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, jana Tarehe 06 Novemba, 2023 kulikuwa na tatizo kubwa la mtandao wa Vodacom. Shughuli nyingi za kutuma fedha zilikwama, mambo mengi yalikwama kabisa, mawasiliano hata kutuma miamala ya fedha kwenye benki na kwenye simu.
Je, Vodacom jana ilipatwa na changamoto gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Kata hizi ambazo Mheshimiwa Waziri amezitaja zimefikia hatua gani, katika utekelezaji wake, maana wameshazipitia tayari, zimefikia hatua gani ili wananchi wa Kata hizi za Ruvu, Msindo, Mshewa, Vudee, Mhezi na Suji waweze kupata mitandao ya simu? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na kipengele cha kwanza ni kweli kabisa, jana kumekuwa na changamoto kupitia mtandao wa Vodacom, tunasema kwamba kulikuwa na technical hiccups. Technical hiccups maana yake kwamba, ilitokea katika network service ambapo iliathiri masuala ya kupiga, sms, pamoja na kutuma pesa kwa mtandao wa M-Pesa, lakini wenzetu wametoa taarifa wanaendelea kuifanyia kazi na leo tumeona kuna improvement, pia wateja ambao waliathirika ni Watanzania milioni 1.8. Kwa hiyo, tunaamini kwamba wanaendelea kulifanyia kazi na baadae watatupatia mrejesho wa hatua ambayo wameifikia na tunaamini kwamba hili tatizo litakuwa limeisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Kata za Ruvu, Msindo, Mshewa, Vudee, Mhezi pamoja na Suji ukiachilia hili suala la Kata ya Tae ambayo tutaiingiza katika mpango wa utekelezaji wa minara mingine inayokuja, hizi Kata ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya kwanza naomba uniruhusu nitoe ufafanuzi kidogo hapa. Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla tumekuwa na maswali mengi sana kuhusiana na minara hii 758, tulichokifanya pale mwanzoni ni kubainisha Kata ambazo zina changamoto ya mawasiliano, lakini hatukubainisha maeneo ya kwenda kujenga minara hii. Kwa hiyo, tunachokifaya ni kuhakiksha kwamba tunaenda kubainisha maeneo sasa ambapo tunaenda kujenga minara na baada ya kufanya hivyo tunaenda kuhakikisha kwamba sasa tunaomba vibali. Wakati haya yote yanaendelea labda nikupe takwimu kidogo kwamba, mpaka sasa Airtel kati ya maeneo 188 mpaka sasa ameshaainisha maeneo 140 ambayo ni zaidi ya asilimia 70.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna TTCL yeye ameshamaliza maeneo yote pia ameshaingia mikataba na wahusika wa maeneo. Tigo kati ya maeneo 137 tayari maeneo 133 yameshakamilika. Halotel maeneo 22 yote ameshakamilisha kulingana na mkataba wake lakini Vodacom maeneo 133 kati ya 137. Kwa hiyo, unaweza ukaona kwamba kuna hatua ambazo Waheshimiwa Wabunge hawatoziona kule zinatokea katika Majimbo yao ni kwa sababu kuna hatua ambazo ni za kiufundi na ni lazima tuzifuate na ni lazima zikamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa tunahitaji minara hii ijengwe kwa kasi, lakini ni lazima tuhakikishe kwamba, tunafuata utaratibu ambao hautakuja kuingiza Taifa katika janga la minara ambayo itajengwa halafu idondoke. Kwa hiyo ni lazima haya yafanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kwamba, kampuni zote mpaka sasa zimeshaandika kuomba vibali na wakati wanaandika kuomba vibali bado wameagiza vifaa kwa ajili ya ujenzi. Kwa hiyo, kuna hatua mbalimbali ambazo zinaendelea kufanyika kuhakikisha kwamba minara hii itakapokuja kuanza kusimamishwa, nakuhakikishia kwamba inaweza ikasimama kwa pamoja na Watanzania, Waheshimiwa Wabunge, wote tutashangilia kazi kubwa ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana lakini kwa ndugu yangu wa Same, bahati nzuri yeye yuko katika minara ya Halotel ambapo wao kazi kubwa imeshafanyika, Halotel wameshaanza kujenga minara mitano. Katika minara hiyo mitano kuna mmoja ambao unajengwa katika Kata ya Mheshimiwa David Mathayo David. Nakushukuru sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved