Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Boniphace Nyangindu Butondo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kishapu
Primary Question
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza:- Je, lini ujenzi wa wodi za wagonjwa, nyumba za Madaktari, maabara na mortuary katika Vituo vya Afya vya Mwanhalanga na Negezi utakamilika?
Supplementary Question 1
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kuipongeza Serikali kwa majibu mazuri kuhusiana na miradi hii miwili Mwanhalanga na Ukenyenge.
Mheshimiwa Spika, ninaomba tu kushukuru kwamba shilingi milioni 500 kwa ajili ya Kituo cha Ukenyenge zilijenga yale majengo matano lakini upungufu bado ni mkubwa sana na hivyo kupelekea Kituo hiki kuendelea kubaki na kutokuwa na hadhi kama Kituo cha Afya. Tunahitaji majengo kwa ajili ya wodi za akina mama na akina baba lakini tunahitaji pia walkways kwa baadhi ya Wodi ambazo zitakuwa zinaunganishwa na hizi njia za kuwafikisha Madaktari na wagonjwa maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kuhusiana na Kituo cha Afya cha Mwanhalanga. Kituo hiki cha afya kina majengo mawili tu na bado wagonjwa ni wengi sana. Ni lini Serikali itakwenda kujenga majengo maalum kwa ajili ya wodi za akina mama, wodi za akina baba, mortuary pamoja na nyumba za watumishi ili tuongeze ari ya watumishi kutenda kazi katika maeneo haya? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Butondo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza napokea pongezi zake kwa Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo kwa kweli imefanyika katika Sekta ya Afya kwa ujenzi wa Vituo vya Afya kikiwemo hiki Kituo cha Afya cha Negezi ambacho kimepokea shilingi milioni 500. Ninamhakishia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunatambua majengo haya bado hayatoshi, hayajakidhi mahitaji, bado tunahitaji wodi, bado tunahitaji mortuary na majengo mengine.
Mheshimiwa Spika, safari ni hatua Mheshimiwa Mbunge, Serikali inaendelea kutenga fedha kwenye bajeti, tuhakikishe kwamba fedha hizi zinapelekwa kwa ajili ya kukamilisha miundombinu hiyo.
Mheshimiwa Spika, pia kuhusiana na Kituo cha Afya cha Mwanhalanga, tunafahamu, tulishapeleka fedha lakini bado kuna majengo ambayo tumeshaweka mpango mkakati kwa ajili ya kutenga fedha ya ukamilishaji. Ahsante.
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza:- Je, lini ujenzi wa wodi za wagonjwa, nyumba za Madaktari, maabara na mortuary katika Vituo vya Afya vya Mwanhalanga na Negezi utakamilika?
Supplementary Question 2
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Mgeta kimejengwa toka mwaka 2018 mpaka leo kimejengwa mortuary imekamilika hakina majokofu manne ya mortuary. Ni lini Serikali itapeleka majokofu manne ya mortuary pamoja na kwamba vituo hivyo vilipewa shilingi milioni 400 ya kujenga na milioni 300 ya vifaa vya tiba...
SPIKA: Umeshauliza swali Mheshimiwa.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Getere, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Mgeta kimejengwa, kimekamilika, kimeanza kutoa huduma lakini jengo la kuhifadhia maiti limekamilika, tayari Serikali imeshapeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Halmashauri ya Bunda. Moja ya kazi ambayo itafanyika ni kununua jokofu kwa ajili ya kuhifadhia maiti katika kituo hiki cha Mgeta. Ahsante.
Name
Michael Constantino Mwakamo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibaha Vijijini
Primary Question
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza:- Je, lini ujenzi wa wodi za wagonjwa, nyumba za Madaktari, maabara na mortuary katika Vituo vya Afya vya Mwanhalanga na Negezi utakamilika?
Supplementary Question 3
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, Kata ya Magendo, Kibaha Vijijini tumepokea jokofu la kuhifadhia maiti lakini mortuary haijajengwa; je, lini tutapata pesa kwa ajili ujenzi?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakamo kuwa Serikali ilishatoa maelekezo kwa Halmashauri zetu kote nchini, kwamba Mheshimiwa Rais anapopeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya, lakini anapopeleka fedha kwa ajili ya vifaatiba, kuna baadhi ya miundombinu ambayo iko ndani ya uwezo wa mapato ya ndani ya Halmashauri kama majengo ya mortuary.
Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kumuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kibaha, kutenga fedha kwenye mapato ya ndani kujenga jengo la mortuary ambalo ni jengo la gharama ya kawaida kabisa ili wananchi waendelee kupata huduma katika eneo hilo. Ahsante.(Makofi)
Name
Esther Nicholus Matiko
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza:- Je, lini ujenzi wa wodi za wagonjwa, nyumba za Madaktari, maabara na mortuary katika Vituo vya Afya vya Mwanhalanga na Negezi utakamilika?
Supplementary Question 4
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, Kata ya Susuni na Mwema zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, hazina kabisa Kituo cha Afya na hivyo kusababisha wananchi kutembea kuja kutafuta huduma Tarime Mjini. Nataka kujua ni lini Serikali itapandisha hadhi Zahanati ya Kiongera ambayo imekarabatiwa ili kuwa Kituo cha Afya na kuweza kurahisisha huduma kwa wananchi hawa?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante, ujenzi wa vituo vya afya katika Kata, tunajenga kimkakati, kwanza kwa kufanya tathmini ya vigezo kwa maana ya idadi ya watu, umbali kutoka kituo kingine, pia maeneo yale ambayo ni magumu kufikika. Kwa kuwa, Kata hii ya Susuni na Mwema hatujapata tathmini yake ya kutosha, naomba tuichukue hoja ya Mheshimiwa Mbunge tukafanye tathmini tuone kama inakidhi vigezo, tuziingize kwenye mpango mkakati, aidha kupandisha hadhi zahanati au kufanya ujenzi katika Kata hizo, ahsante.