Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka ruzuku kwenye nishati ya gesi ili wananchi waweze kumudu kununua?
Supplementary Question 1
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, naomba niulize swali moja dogo lenye sehemu (a), (b), (c), (d) kama ifuatavyo: -
SPIKA: Mheshimiwa ni (a) na (b) pekee. Kwa hiyo, katika hayo manne chagua mawili.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongea na wadau ili waweze kuondoa gharama kubwa iliyopo ya ununuzi wa mtungi wa gesi na gesi yenyewe, wakati mchakato wa kupunguza au kuweka ruzuku kwenye nishati ya gesi unaendelea kwa Serikali?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Shule ya Ufundi Mtwara Tech. imefunga mfumo wa gesi asilia suala ambalo limepunguza gharama kubwa ambayo ilikuwa inatumika wakati wakitumia nishati mbadala ya kuni na mkaa. Wakati wakitumia nishati hiyo walikuwa wanatumia shilingi milioni saba. Sasa baada ya kuweka mfumo wanatumia shilingi milioni 1.8.
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka mfumo huo kwenye Taasisi zote za Serikali ikiwemo Chuo cha Ualimu Matogolo na Shule za Sekondari zote katika Mkoa wa Ruvuma na nchi yote ya Tanzania? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyofuatilia matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la ruzuku, ajenda ya nishati safi ya kupikia ni ajenda ya Mheshimiwa Rais mwenyewe. Wote mnakumbuka wakati wa mkutano wa COP28 Dubai, alizindua Mkakati wa Nishati ya Kupikia kwa Wanawake Afrika. Kwa hiyo, jambo hili tumelibeba kwa uzito sana.
Mheshimiwa Spika, kuhusu ruzuku tayari tuna programu na miradi kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya tunayo programu ambapo mawakala wanawezeshwa kifedha ili kupunguza bei ya mitungi kwa wale wanunuaji wanaonunua gesi kwa mara ya kwanza. Tutaendelea kubuni miradi na kutafuta fedha ili kuhakikisha wananchi wanapata mitungi ya gesi kwa gharama rahisi zaidi.
Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusiana na kuwekeza mifumo ya gesi katika taasisi; kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) tumeshaanza mradi kwa ajili ya kuweka nishati hii safi ya kupikia ya gesi kwenye magereza, kambi za Jeshi pamoja na shule za msingi na sekondari. Tutaendelea kutafuta fedha ili kuhakikisha tumefikia taasisi nyingi zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa taasisi alizosema za Mkoa wa Ruvuma tutazingatia pia, ili kuhakikisha wanawekewa mifumo hii, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved