Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Primary Question

MHE. DEO K. SANGA (K.n.y. MHE. PROF. NORMAN A. S. KING) aliuliza:- Shamba la Mifugo la Kitulo lililoko Wilaya ya Makete lilianzishwa kwa madhumuni ya kuwezesha wananchi kupata ndama na maziwa kwa ajili ya kukuza uchumi wao, lakini cha kusikitisha, uzalishaji wa ng‟ombe katika shamba hilo kwa sasa umepungua sana kutokana na Serikali kushindwa kusaidia kuimarisha shamba hilo:- Je, Serikali inafanya jitihada gani kuimarisha shamba hilo ili liweze kusaidia wananchi wa Makete na Mikoa ya jirani kupata ng‟ombe na kukuza uchumi wao?

Supplementary Question 1

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Wilaya ya Makete ndipo ambapo kituo kinachozalisha mitamba katika wilaya hiyo na wananchi wa Wilaya ya Makete ndiyo wamekuwa miongoni mwa wanaofaidi na mikoa mingine jirani kama alivyosema:-
Swali, hivi sasa Serikali imejipangaje kuona sasa Halmashauri jirani za Mkoa wa Njombe hususan Wilaya ya Wanging‟ombe, Njombe, Ludewa, Halmashauri ya Mji wa Makambako na Lupembe zinafaidika kupata mikopo ya kuwakopesha mitamba hii ili iweze kuzalisha katika halmashauri hizi wananchi waweze kunufaika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Makete walitoa eneo kubwa sana kwa kituo hiki na eneo hilo bado kubwa halitumiki, Serikali imejipangaje kuona wananchi wa Wilaya ya Makete wanakopeshwa mitamba hii ili waweze kupata eneo ambalo limekaa tu halitumiki waweze kunufaika nalo? (Makofi)

Name

William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni namna gani Serikali imejipanga kutoa fursa kwa wananchi wa Halmashauri ambazo zimepakana na shamba ili kujipatia mikopo kwa ajili ya kuweza kujiendeleza katika ufugaji; Wizara ipo tayari kushirikiana na Halmashauri hizo ili waweze kuona fursa zilizopo katika Benki ya Kilimo, lakini vilevile katika Benki ya TIB na NMB ili waweze kupata fursa ya kupata mikopo na kuwekeza katika ufugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kama Wizara ina mpango wa kugawa ardhi kwa wananchi wanaozunguka shamba hilo; napenda kusema kwamba pamoja na Serikali kutambua umuhimu wa Sekta Binafsi na wananchi mmoja mmoja kujihusisha katika ufugaji; kwa sasa Serikali inaona kwamba ni vizuri shamba hilo likaendelea kubakia mikononi mwa Wizara ili liweze kutumika kwa ajili ya watu wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Wizara inatambua kwamba huko nyuma jitihada za kubinafsisha ardhi pamoja na mali nyingine za Wizara, hazijazaa matunda makubwa sana; na mpaka leo hii viwanda vya nyama ambavyo tumebinafsisha pamoja na viwanda vya ngozi, lakini vilevile blocks za ranchi za Taifa, uzoefu umetuonesha kwamba hatujapata mafanikio makubwa sana katika kuendeleza Sekta ya Mifugo kwa utaratibu huo.
Kwa hiyo, Serikali na Wizara inalenga kuwekeza zaidi katika mashamba hayo na katika sekta kwa kusimamia yenyewe badala ya kubinafsisha mashamba hayo.