Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:- Je, zabuni ngapi zilitolewa na Halmashauri za Majiji, Manispaa na Wilaya kwa makundi maalum hasa wanawake kama sheria inavyotaka?

Supplementary Question 1

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini inaonekana dhahiri kwamba waliopata ni wachache sana na hapo inaonesha kwamba uelewa ni mdogo: Je, Serikali ina mpango gani sasa kupeleka elimu hii katika ngazi za chini za Kata?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa fedha hizo zipo lakini haziendi kama inavyotakiwa na wahusika hawazipati, ni lini sasa Serikali itaweka nguvu kubwa ili wote waweze kupata kwa wakati? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shally Raymond, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba uelewa katika jamii yetu na hasa makundi ya wanawake vijana na watu wenye ulemavu kutumia fursa ya asilimia 30 ya zabuni bado iko chini. Mpango wa Serikali, kwanza tumeendelea kutoa elimu katika jamii kupitia Maafisa wa Maendeleo ya Jamii na pia tumeelekeza Wakurugenzi na Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji kuwa ajenda hiyo ni ya kudumu katika vikao vyote vya vijiji ili wananchi wapate uelewa waweze kutumia fursa hii ya asilimia 30 ya zabuni.

Mheshimiwa Spika, pili, ni kwamba kweli fedha zipo, lakini haya makundi hayapati, sababu ni ile ile kwamba wengi hawajajiunga kwenye vikundi vile, lakini baadhi ya vikundi havina sifa na Serikali itaendelea kuhamasisha ili wajiunge na kutumia fursa hiyo ipasavyo, ahsante.

Name

Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:- Je, zabuni ngapi zilitolewa na Halmashauri za Majiji, Manispaa na Wilaya kwa makundi maalum hasa wanawake kama sheria inavyotaka?

Supplementary Question 2

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na changamoto alizozisema Naibu Waziri za makundi hayo, bado vile vikundi vichache vilivyofanikiwa kupata zabuni havikuweza kulipa kwa wakati licha ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kueleza changamoto ya kutolipa hayo madeni kwa wakati. Nini mkakati mahususi wa kusaidia kulipa hizo fedha na hasa haya makundi mahususi ili kupunguza adha ya umasikini na kuendelea kufanya biashara.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Serikali imeweka mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba tunawapa kipaumbele Makundi haya Maalum yanapopata zabuni ya asilimia 30 kulipwa mapema zaidi; kwa sababu tunajua kwamba ni makundi ambayo hayana mtaji wa kutosha.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha inatoa kipaumbele na pale wanapomaliza zabuni zao wanapata malipo ili waweze kuendelea kufanya shughuli za ukandarasi au shughuli nyingine kwa ufanisi zaidi.