Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Martha Festo Mariki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza:- Je, lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa Shule ya Sayansi ya Wasichana Mkoani Katavi?

Supplementary Question 1

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kuona umuhimu na kutoa hizo shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa shule ya wasichana nchi nzima. Mkoa wetu wa Katavi unaongoza sana kwa mimba za utotoni, vile vile katika shule zetu za sekondari kuna upungufu mkubwa sana wa mabweni kwa ajili ya watoto wa kike; je, upi mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba unajenga mabweni kwa ajili ya kuwanusuru watoto wa kike na mimba za shuleni na utotoni? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, katika elimu ya msingi, kuna shule zilizojengwa miaka ya 1970 ambazo zimekuwa chakavu sana; pamoja na jitihada za Serikali kutuletea pesa za BOOST, lakini shule nyingi sana bado ni chakavu na zinavuja maji hususan wakati wa masika. Je, upi mkakati wa Serikali kukarabati shule kongwe nchini kuweza kuwa katika level nzuri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mariki. Swali la kwanza juu ya uhitaji wa mabweni katika Shule za Sekondari Mkoa wa Katavi, katika mwaka huu wa fedha ambao tupo sasa unatekelezwa, Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 7.04 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na tayari kuna mabweni 60 ambayo yamejengwa maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo katika Mkoa wa Katavi. Serikali itaendelea kutafuta fedha ya kuweza kujenga mabweni haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha katika fedha zao za miradi ya maendeleo wanajenga mabweni katika Shule za Sekondari ambazo Serikali Kuu, Serikali hii ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imepeleka fedha nyingi katika ujenzi wa shule hizi za sekondari kote nchini, ukiwemo Mkoa ule wa Katavi anakotoka Mheshimiwa Mariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili, kwanza nikiri kwamba Mheshimiwa Martha amekuwa akilifuatilia sana jambo hili na amekuja mara kadhaa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuulizia juu ya shule hizi kongwe za msingi katika Mkoa wa Katavi. Tayari Serikali kupitia Mradi wa BOOST ilijenga shule 302 kote nchini. Hii ni kwa mara ya kwanza kwa kipindi kirefu sana ambapo Serikali inawekeza fedha nyingi zaidi ya shilingi bilioni 230, katika shule za msingi. Hii inaonesha ni namna gani Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka kipaumbele katika shule zetu za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shule kongwe hizi kuna madarasa zaidi ya 3,350 ambayo yamejengwa nchi nzima kupitia mradi huu wa BOOST ikiwemo katika maeneo mengine shule kongwe na Mkoa wa Katavi nao walipata madarasa katika mgao huu wa madarasa 3,350. Serikali itaendelea kutafuta fedha zaidi kwa ajili ya kuweza kujenga shule au kukarabati shule kongwe zilizopo hasa zile za msingi. (Makofi)