Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Bonnah Ladislaus Kamoli
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Segerea
Primary Question
MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza:- Je, lini kanuni mpya za malipo ya pensheni kwa wastaafu ya kila mwezi ya kutoka asilimia 50 mpaka 67 zitaanza kutumika?
Supplementary Question 1
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini bado kuna baadhi ya wastaafu wanalalamika kwamba hawapati hayo mafao yao. Pia wastaafu ambao wapo Zanzibar tayari wameshaongezewa, kutokana na kiwango walichokuwa wanapata kimeongezewa.
Je, Serikali ina mpango gani hapa kwetu Tanzania Bara ili na wenyewe waweze kuongezewa hayo mafao?
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la kwamba kuna watu ambao hawapati. Lazima tukiri na kuwa wawazi kwa kazi nzuri ambayo ameifanya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, kulikuwa kuna changamoto kubwa awali na tunakiri hilo kwa sababu ya mifuko kuwa mingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tulijaribu kufanya ile harmonization, ambayo ilipelekea kwenda kutengeneza mfumo huu wa kikokotoo kipya ambapo kwa sasa ukiangalia mkupuo wa mafao tunalipa kwa asilimia 50 mpaka 67 na ile pensheni ya kila mwezi imetoka asilimia 25 kwenda 33. Sasa malipo hayo kwa sasa mifuko imekuwa ikilipa ndani ya siku 30. Inalipwa kama nyaraka zote na kila kitu kimekamilika hata kabla ya siku kumi mtu anakuwa amepata mafao yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, changamoto ya mafao kwa sasa hatuna kama Mheshimiwa Mbunge anayo anaweza kutupatia. Kwa upande wa Zanzibar suala la mifuko siyo la kimuungano. Kule wenzetu wametangulia tunawapongeza kwa kazi hiyo. Sisi tupo tayari kwenye hatua nzuri ya kufanya actuarial evaluation, ambayo itatusaidia kule taarifa ambayo itaangalia ustahimilivu wa mifuko na kiwango cha upatikanaji wa mafao kama kimepanda. Basi tunakwenda kufanya maboresho hayo na hilo litakuwa ni zoezi la haraka na tayari miaka mitatu ya kufanya evaluation hiyo imeshatimia na tuko kwenye zoezi hilo, ahsante.
Name
Ndaisaba George Ruhoro
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngara
Primary Question
MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza:- Je, lini kanuni mpya za malipo ya pensheni kwa wastaafu ya kila mwezi ya kutoka asilimia 50 mpaka 67 zitaanza kutumika?
Supplementary Question 2
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana; watumishi wengi nchini wameendelea kulalamikia sana suala la kikokotoo. Hii ni kwa sababu kikokotoo kinasababisha wachukue mafao kidogo yale ya awali.
Ni upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha inaboresha kanuni ya kikokotoo ili kuwafanya watumishi wengi hasa walimu wapate mafao mengi ya mkupuo ya awali? Ahsante. (Makofi)
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisaba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya msingi lakini pia kwenye maelezo yangu na ufafanuzi wa awali. Mkupuo wa awali tulikuwa tunalipa asilimia 25 kwa sasa tumefika asilimia 33. Mungu jalia mbele kwa jitihada anazofanya Mheshimiwa Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan, tutaenda hata zaidi ya asilimia hizo. Pensheni ya mwezi tulikuwa asilimia 50 sasa tumefika asilimia 57. Utaona hiyo level of growth ambayo ni kubwa sana na ni supersonic speed ya kuweza kuhakikisha kwamba wafanyakazi wastaafu wanapata mafao yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi katika hilo Mheshimiwa Rais, ameonesha dhamira yake ya dhati sana. Ni kipenzi cha wafanyakazi na Vyama vya Wafanyakazi. Wakati wote tumekuwa tukikutana katika utatu kwa maana ya Serikali, Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri, kwa ajili ya kuona namna gani tunaweza kufanya maboresho haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza kuona hata kwenye kipindi cha Korona na mazingira magumu tumeweza kupandisha asilimia…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, malizia hilo. Umeshamjibu vizuri. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved