Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kavejuru Eliadory Felix

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buhigwe

Primary Question

MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: - Je, biashara ya Kaboni katika misitu ya asili na ya kupanda imechangia kiasi gani kwenye pato la Taifa tangu iingie nchini?

Supplementary Question 1

MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niishukuru Serikali kwa majibu mazuri; pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

(a) Je, Serikali ina mkakati gani ya kutoa elimu ihusuyo biashara ya kaboni kwa wananchi wanaozunguka hifadhi za misitu hapa nchini?

(b) Kwa kuwa biashara ni matangazo, je, Serikali inatumia njia gani kutangaza misitu yetu yote nchini ambayo idadi yake ni 589 kwa makampuni ya kigeni yanayojishughulisha na biashara ya kaboni?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felix, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue fursa hii kumpongeza Ndugu yangu, Mheshimiwa Felix Kavejuru kwa kazi kubwa anayoifanya kwa sababu katika ajenda hii si mara moja tu hata katika side meetings tunazofanya amekuwa kipaumbele sana kugombania Mkoa wa Kigoma na hasa Halmashauri yake ya Buhigwe katika suala zima la biashara hii ya kaboni.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati uliokuwepo ni kwamba tumefanya mkutano na Wakuu wote wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha tunapeleka meseji hii ya biashara ya kaboni. Bahati nzuri zoezi hili linakwenda vizuri, na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara nyingine za kisekta na hasa Ofisi ya Maliasili ambayo vile vile kwa pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumekuwa tukishirikiana katika suala zima la kupeleka juu hii elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kupitia vyombo vyetu mbalimbali vya habari tumeweza sasa hivi kuanza kutoa elimu hii kwa watu wajue kwamba kuna fursa hii kubwa ya biashara ya kaboni. Kwa hiyo huu ndiyo mkakati ambao tunaendelea nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunatumia fursa hii kuitangaza; na hasa nishukuru sana katika mkutano tuliofanya mwaka huu kule Dubai (Cop 28) miongoni mwa jambo kubwa ambalo tulitangaza kwa wadau mbalimbali wawekezaji katika suala zima la biashara ya kaboni. Naomba niwahakikishie Watanzania, mpaka hivi sasa mwitiko wa wawekezaji ni mkubwa na wengi wamejitokeza. Sasa niwaombe hasa Waheshimiwa Wabunge, kwamba tutumie fursa hii hasa katika maeneo yetu ili tuone kwamba hili ni eneo kubwa sana ambalo tunaweza tukapata pato la kuongeza mapato ya halmashauri zetu na katika Pato la Taifa.