Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ally Anyigulile Jumbe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Primary Question

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza: - Je, lini ujenzi wa Kituo cha Umeme (substation) utaanza Kyela?

Supplementary Question 1

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza naipongeza Serikali kwa juhudi kubwa inazofanya kuhakikisha umeme unapatikana. Wananchi wa Kyela wamekuwa ni wavumilivu sana kwa muda mrefu, umeme pamoja na ratiba ya mgao wa umeme, lakini bado kuna hitilafu za umeme ambazo zinatokea mbeya na Rungwe zinawaathiri wananchi wale. Je, Serikali haioni sasa kwamba ni wakati muafaka kuachana na mlolongo mrefu huu wa upembuzi yakinifu na kuleta mambo mengine yanayoathiri uharakishaji wa ujenzi wa kituo hiki cha umeme? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, miaka ya nyuma ya 1990, umeme Kyela ulikuwa unatoka pale Kiwira Coal Mine na wananchi wa Kyela walikuwa wanapata umeme bora kabisa, lakini sasa hivi umeme huo haufanyi kazi na haupo. Kwa kuwa tarehe 10 Agosti, 2021 TANESCO iliingia makubaliano na STAMICO ili wazalishe megawat 200 ambazo zingetokea Kyela moja kwa moja, je, Serikali haioni sasa kwamba ni wakati muafaka wa kuharakisha kuanza kwa mradi huu? (Makofi)

Name

Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaelewa kadhia wanayopata wananchi wa Jimbo lake la kukatika kwa umeme mara kwa mara. Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha changamoto hizi zinaondoka, lakini hitimisho la muda mrefu ni ujenzi wa kile kituo cha kupoza umeme katika Wilaya ya Kyela. Kama nilivyosema, mradi huu ni sehemu ya mradi wa gridi imara ambapo katika kipindi hiki Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 470 kuhakikisha mradi ule unaweza kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuhusu kuharakisha na kuachana na mlolongo, hatua hizi zinazofanyika sasa za upembuzi yakinifu, kufanya tathmini ya maeneo ya wananchi ambayo yakichukuliwa watahitajika kufidiwa na mambo kama hayo, ni hatua muhimu sana ili mwisho wa siku tuweze kupata mradi ambao hautakuwa na matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira Serikali imejidhatiti kuhakikisha kwamba ndani ya kipindi kifupi kama tulivyosema mradi huu unatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu jibu lake la swali la pili ni kweli kwamba pale kuna mradi wa makaa ya mawe unaokusudiwa kujengwa kati ya TANESCO na wenzetu wa STAMICO. Nafurahi kusema kwamba, mwezi uliopita wataalam wa TANESCO na STAMICO wamekaa na kukubaliana kuharakisha mchakato wa ujenzi wa mradi huu katika kupitia upembuzi yakinifu uliofanyika ili kuakisi mahitaji ya sasa. Takribani shilingi milioni 400 zimetengwa kwa ajili ya kuharakisha kazi hiyo. Nimuombe awe na subira tunauhitaji sana mradi huu.