Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Primary Question
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza: - Je, lini Serikali itamaliza ujenzi wa Bwalo katika Sekondari ya Malagarasi - Muhambwe lililosimama tangu mwaka 2017?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwanza nashukuru Serikali kwa kutenga fedha hizi kwa ajili ya kumalizia bwalo hili la Shule ya Malagarasi, hata hivyo, nina maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; shule hii imeanza mwaka 1995 baada ya wananchi kujenga madarasa sita, madarasa haya hayajawahi kufanyiwa ukarabati. Je, ni lini Serikali itatenga fedha ili kukarabati madarasa ya shule hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; shule hii ina zaidi ya wanafunzi 1,240 ikiwa ni kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita na wanafunzi takribani 418 wa kidato cha sita hawana mabweni. Je, ni lini Serikali itajenga mabweni angalau mawili kwa ajili ya mabinti wetu katika shule hii?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyowapambania wananchi wake. Swali lake la kwanza, kuhusu ukarabati wa madarasa chakavu, napenda Mheshimiwa Mbunge afahamu kwamba Serikali inatambua uwepo wa shule chakavu za msingi na sekondari na ndio maana Serikali tayari imeshaanza ukarabati wa shule hizo kupitia miradi ya EP4R, SEQUIP na BOOST. Serikali kwa kutambua uhitaji na kwa kadri fedha zitakapokuwa zikipatikana, Serikali inakusudia kuja kufanya marekebisho katika shule yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, ambapo Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kuhusu ujenzi wa mabweni na hasa kwa wasichana. Mheshimiwa Mbunge naomba ufahamu Serikali inatambua kwamba kuna umuhimu wa kupata mabweni na hasa kwa watoto wa kike na ndio maana Serikali ilianza ujenzi wa shule za sekondari za bweni za wasichana katika kila mkoa kupitia Mradi wa SEQUIP. Kwa hiyo, kwa kuzingatia umuhimu wa kuwa na mabweni na hasa kwa watoto wa kike Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni hayo. Ahsante. (Makofi)
Name
Jackson Gedion Kiswaga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Primary Question
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza: - Je, lini Serikali itamaliza ujenzi wa Bwalo katika Sekondari ya Malagarasi - Muhambwe lililosimama tangu mwaka 2017?
Supplementary Question 2
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja fupi. Shule ya Msingi Igumila madarasa yake mawili yamebomoka na Naibu Waziri Utumishi alipopita pale alituahidi kutupa madarasa mawili. Je, ni lini fedha hizo zitapelekwa ili turejeshe hayo madarasa mawili?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyoomba Mheshimiwa Mbunge kutambua uhitaji wa madarasa katika Shule ya Msingi Igumila, Serikali inaendelea kuangalia vipaumbele na kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali itafanya jitahada kwa kadri fedha zinavyopatikana iweze kujenga madarasa haya. Ahsante
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved