Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Primary Question

MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:- Je, Serikali imetoa na kukusanya kiasi gani kutokana na mkopo wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi na kiasi gani kimerudi kuendeleza mpango huo?

Supplementary Question 1

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Migogoro ya ardhi inazidi kushamiri katika maeneo mbalimbali hasa katika Wilaya ya Kilosa hususani Jimbo la Mikumi. Fedha hizi zilikuwa ni mpango endelevu kwa maana ya revolving fund, sehemu ya mwisho ya swali langu lilikuwa ni kwamba; je, fedha iliyorudi ni kiasi gani ambacho kimeendelea kukopeshwa kwenye halmashauri? Swali hilo halikujibiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza; je, ni lini fedha zaidi ya bilioni 30 ambazo zimekopeshwa na kwenda kwenye matumizi mengine ambayo hayakukusudiwa, kwa mfano fidia, ujenzi wa mahoteli na miundombinu mingine ambayo siyo lengo la fedha hizi, watuhumiwa ama waliopeleka fedha hizo watachukuliwa hatua?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni lini Serikali itazisimamia fedha hizi ambazo ni revolving fund ili faida yake irudi kupima maeneo mengine?

Name

Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba fedha hizi zote zilizotolewa zinarejeshwa. La kwanza, ipo mipango ambayo imekwishapangwa ikiwemo kutolewa kwa mwongozo maalum wa jinsi ya utoaji na urejeshaji wa fedha hizo baada ya kugundua kwamba yako baadhi au ziko baadhi ya halmashauri ambazo zimekwenda kinyume na utaratibu ule ambao ulitolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba mwongozo upo tayari kwa ajili ya kutoa hizo pesa kwa ajili ya halmashauri nyingine. Pia, kwa zile halmashauri ambazo hazijatoa tumekwishafanya mazungumzo pamoja na wenzetu wa USEMI ambao ni Kamati yako ya Bunge ili kuweza kuona kwamba kwa zile halmashauri ambazo hazijarejesha pesa zinaitwa mbele ya Kamati hiyo tukishirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili ziweze kurejesha pesa hizo kama ambavyo imekubalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo kwa zile halmashauri katika swali lake la pili halmashauri ambazo hazijarejesha pesa ni hatua gani ambazo zinachukuliwa? Tumeshawasiliana na halmashauri hizo na tumeshazielekeza halmashauri hizo na kupeana muda zikiwemo halmashauri ambazo mpaka sasa hivi zimerejesha sehemu ya pesa hizo ambazo ni halmashauri 43 na zile halmashauri mbili ambazo hazijarejesha nazo zihakikishe kwamba fedha zimekuja ndani ya muda. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Primary Question

MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:- Je, Serikali imetoa na kukusanya kiasi gani kutokana na mkopo wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi na kiasi gani kimerudi kuendeleza mpango huo?

Supplementary Question 2

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa zipo halmashauri ambazo zimefanya vizuri kwa kurejesha fedha hizo ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Mwanza. Je, Serikali ina mpango gani wa kuziongezea mkopo halmashauri hizi ili ziweze kufanya kazi hii ya kupanga, kupima na kumilikisha kwa uzuri zaidi?

Name

Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama inavyofahamika Mfuko huu ni Mfuko ambao fedha zake ni fedha za kuzungushwa. Kwa maana hiyo, kwa zile halmashauri ambazo zitakuwa zimefanya vizuri kwa kufanya marejesho vizuri na ndani ya muda, maelekezo ya mwongozo tulioutoa ni kuhakikisha kwamba halmashauri hizi zinabuni tena miradi na fedha hizi zinapelekwa katika halmashauri hizo ili kuendelea kuzalisha viwanja na kutengeneza makazi kwa ajili ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba, kwa zile halmashauri ambazo zimekwishakamilisha kurejesha fedha hizo tunawakaribisha ndani ya ofisi yetu ili tuweze kuendelea kuwakopesha ili waweze kupima ardhi, kupanga na kutengeneza utaratibu mzuri kwa ajili ya makazi yaliyo bora kwa wananchi wa Tanzania kama ambavyo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza kupitia Mradi huu wa Kupanga, Kupima na Kurasimisha Ardhi ya Tanzania. (Makofi)