Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:- Je, lini Serikali itasimamia ushushaji wa bei ya mbegu za mahindi kwa wakulima?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali na nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; bei elekezi ambazo zilitangazwa na TOSCI tarehe 20 Oktoba, 2023 ambayo ni shilingi 4,000 kwa kilo kwa mbegu zinazochavushwa huria au OPV na shilingi 7,150 hadi 8,000 kwa mbegu chotara, hili ndilo linalolalamikiwa na wananchi kwamba ni bei kubwa sana. Je, kwa nini Serikali haiweki ruzuku? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kazi ya utafiti wa mbegu ni kazi ya msingi ya Serikali. Kwa nini hadi sasa mbegu 60% bado zinatoka nje? (Makofi)

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kakunda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza siyo sahihi kusema kwamba 60% ya mbegu zinazouzwa katika soko letu zinatoka nje. Mwaka huu kama nchi mbegu zinazotoka nje na mbegu zilizozalishwa ndani ya nchi jumla ilikuwa ni tani 60,000, ambapo tani 17,000 zimetoka nje na tani 43,000 zimezalishwa ndani ya nchi na asilimia 80 ya hizi tani 43,000 zimezalishwa na Makampuni ya Kitanzania na mbegu za msingi zimezalishwa kutoka TARI katika Taasisi yetu ya Utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo amesema ni suala la ruzuku. Kwanza kabla ya bei elekezi mbegu ambazo zilikuwa zimetangazwa na Serikali kuuzwa shilingi 4,000 zilikuwa zinauzwa kati ya shilingi 20,000 mpaka 25,000 katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu kwa kilo mbili. Kwa maana ya wastani wa shilingi 12,000, lakini baada ya bei elekezi ya Serikali zimeuzwa kwa shilingi 7,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, nalipokea wazo lake la kwamba kwa nini Serikali isiweke ruzuku katika mbegu? Wizara sasa hivi inafanya tathmini ya kutengeneza mjengeko wa bei na mabadiliko ya Kanuni ya TOSCI ili Mamlaka ya TOSCI ipewe haki ya kisheria ya kuweza kusimamia suala la udhibiti wa bei. Kwa hiyo niwaombe Waheshimiwa Wabunge watupe muda, tutaangalia mfumo mzuri wa kusaidia sekta ndogo ya mbegu na tunaelewa umuhimu wa Serikali kuweka ruzuku kama tulivyoweka kwenye mbolea. (Makofi)

Name

Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Primary Question

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:- Je, lini Serikali itasimamia ushushaji wa bei ya mbegu za mahindi kwa wakulima?

Supplementary Question 2

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kuchukua hatua nyingi na kuhakikisha kwamba pembejeo zinazifika kwa wakati; je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba cotton twine na jute twine zinafika kwa wakati na pia zinauzwa kwa bei iliyopangwa? (Makofi)

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mama Sitta, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri kumetokea changamoto msimu huu wa tumbaku cotton twine na jute twine zilichelewa na changamoto ya msingi kwa nini zilichelewa Vyama Vikuu vya Ushirika vilichelewa kupata letter of credit kutoka Taasisi za Fedha, hatukuwa na tatizo hili katika misimu miwili, mitatu iliyopita. Nataka niwaahidi wakulima wa tumbaku na Waheshimiwa Wabunge wote wanaotoka katika maeneo ya tumbaku kama tulivyorekebisha mfumo wa upatikanaji wa mbolea na kufika kwa wakati; tutahakikisha tatizo lililojitokeza mwaka huu la cotton twine na jute twine halitokei kwa sababu tumeshaanza kuongea na viwanda vya ndani vya Watanzania ili viwekeze kwenye eneo la kuzalisha cotton twine kwa sababu pamba inapatikana ndani ya nchi. Majaribio ya awali yameanza Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo waweze kuzalisha cotton twine na tuache kutumia dola milioni nne kuagiza kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie Bunge lako Tukufu kuwataka ginners na wanaoongeza thamani kwenye pamba, Serikali ipo tayari kumpa mwekezaji yeyote concession agreement ya muda mrefu, kwa ajili ya kuzalisha cotton twine na atapata mkataba wa muda mrefu na hatuta-import cotton twine kama atawekeza katika eneo hilo. (Makofi)