Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ally Mohamed Kassinge
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilwa Kusini
Primary Question
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza:- Je, Serikali imefikia hatua gani kuwalipa fidia wananchi 438 waliofanyiwa uthamini ili kupisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege Kilwa Masoko?
Supplementary Question 1
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nipate faraja kidogo kwa majibu ya Serikali kwamba hatua iliyofikiwa sasa hivi ni kwamba tayari daftari lipo kwa Mthamini Mkuu Hazina kwa maana ya Wizara ya Fedha. Wananchi hawa wamekuwa wakiathirika kwa muda mrefu tangu 2013 walikuwa ni 144, ukafanyika tena uthamini 2023 wakafikia wananchi 438. Hivi tunavyozungumza wananchi wangu hawa 438, hawana makazi kutokana na kushindwa kuziendeleza nyumba zao kwa kusubiri taratibu za Serikali. Hali ni tete kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kutokana na ukweli kwamba tumeshakaa na Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara ya Fedha na kukubaliana kwamba, wananchi hao walipwe haraka iwezekanavyo. Je, ni nini kauli ya Serikali kulipa wananchi hawa fidia ndani ya kipindi kifupi kijacho kabla hawajaendelea kuathirika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko ni moingoni mwa viwanja 12 ambavyo tuliviingiza katika mpango wa miaka mitano wa kuboresha na kupanua. Faraja tuliyonayo pale Kilwa Masoko tunajenga Bandari ya Uvuvi. Kufuatia ujenzi wa Bandari ya Uvuvi, umuhimu mkubwa wa kuimarisha kiwanja hiki upo na uhitaji mkubwa utahitajika huko mbele ya safari. Je, ni lini sasa Serikali baada ya kulipa wananchi wangu ndani ya muda mfupi, itaanza ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Kilwa Masoko? (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Ally Kassinge kwa ufuatiliaji makini wa Kiwanja hiki cha Ndege. Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa Kiwanja cha Ndege cha Kilwa Masoko. Moja, ameeleza vizuri sana, Serikali imewekeza bilioni 268 kwa ajili ya ujenzi wa bandari kubwa katika Ukanda wetu wa East Africa, Bandari ya Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunao Mradi mkubwa sana wa Gesi wa Mkoa wa Lindi. Hivyo, kiwanja hiki ni muhimu sana siyo tu kwa wananchi wa Lindi na ukanda huo, lakini kwa Taifa letu. Hivyo nimhakikishie Mbunge kwamba, Serikali kauli yake imeshafanya uthamini hatua ya kwanza na ya pili na mpaka wamefika wananchi karibu 454 ambao tunategemea kuwalipa karibu 6,200,000,000. Naomba Mbunge apokee kauli ya Serikali ninayoenda kuitamka sasa. Serikali italipa fidia wananchi hao, mara tu itakapokamilisha hatua za ndani na itaanza hatua za ujenzi mara moja.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri mwenye pesa kasimama.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri mwenzangu kwa majibu yake mazuri, pia nimpongeze sana muuliza swali. Muuliza swali amehusisha Wizara ya Fedha. Ni kweli suala hili tunalitambua na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake kule Kilwa, wawe na amani kabisa fedha hiyo italipwa kwa wakati. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved