Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kulipa fedha za madaraka kwa Waganga Wafawidhi wa vituo vya afya na zahanati nchini?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Naishukuru Serikali kwamba sasa inaenda kuwalipa posho ya madaraka Waganga Wafawidhi wa Zahanati na Vituo vya Afya kama inavyofanya kwa Walimu wa Sekondari pamoja na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi.

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza, kwanza naipongeza Serikali kwa kuendelea kuwalipa posho ya madaraka Watendaji wa Vijiji, japo kuna kusuasua kutokana na udhaifu wa baadhi ya Watendaji lakini kutokana na mapato madogo ya Halmashauri husika. Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya Halmashauri ambazo hazina uwezo kuanza kupata hizo posho kutoka kwa Serikali Kuu, kama ambavyo inafanya kwa Waheshimiwa Madiwani?

Mheshimiwa Spika, swali namba mbili, tunajua vizuri sana kazi kubwa na nzito wanayoifanya Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Mitaa. Je, Serikali haioni kama kuna haja ya hawa Watendaji wa Vijiji na Mitaa kulipwa posho ya madaraka? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nipokee pongezi za Mheshimiwa Mbunge, kwa Serikali kwa kazi kubwa ambayo inafanywa, lakini nimhakikishie tu kwamba, kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi kwamba linafanyiwa kazi na baada ya kufanyiwa tathmini na Wizara ya Utumishi, Menejimenti na Utawala Bora, basi tutaona namna gani tunakwenda kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na posho za Watendaji wa Kata. Serikali ilishaanza kulipa Watendaji wa Kata posho kila mwezi na nitumie fursa hii kusisitiza Wakurugenzi wa halmashauri, kote nchini ambao hawajawalipa Watendaji wa Kata posho zao, wawalipe mara moja kwa sababu zimeshaingizwa kwenye bajeti na ni haki yao kulipwa na ni wajibu wa Wakurugenzi kuhakikisha wanawalipa. Sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutafuatilia na kuchukua hatua pale ambapo tutathibitisha kwamba kuna Mkurugenzi hajalipa posho hizo.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na posho za Maafisa Watendaji wa Vijiji na Mitaa. Naomba niseme kwamba bado tuna mzigo mkubwa sana wa kulipa posho kwa wataalam wetu, tunatambua kazi kubwa inayofanywa na Watendaji wa Vijiji na Mitaa. Niombe kwanza tulichukue hili tukalifanyie tathmini kuona uwezekano na uwezo wa kibajeti kulitizama huko kwa siku za usoni, ahsante.