Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Venant Daud Protas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Primary Question
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: - Je, lini Serikali itaajiri Maafisa Mifugo katika kila Kata ili kuwasaidia wafugaji?
Supplementary Question 1
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, amekiri kila kata, kila Kijiji ni lazima kuwepo na Maafisa Ugani, pamoja na kutoa ajira na kuajiri, kwa nini Maafisa Ugani wanakwenda kuwekwa sehemu ambayo hawana uhitaji? Kwa mfano, unampeleka Afisa Ugani Kata za Dar es Salaam, Kata za Arusha, kwa nini wale wa kule msifanye reshuffle mkawapeleka vijijini ili wakawasaidie wafugaji wetu ambao ng’ombe wao wanapata adha kubwa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kumekuwa na tozo nyingi kwa wafugaji wetu kwa sababu ya kukosa elimu na Maafisa Ugani. Je, kama Serikali hamuoni kwamba mtengeneze mkakati mziondoe zile tozo, msaidie wale wafugaji ili sasa wafurahie matunda ya Serikali yao?
Name
Alexander Pastory Mnyeti
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Misungwi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nianze na hili la kuwaweka Maafisa Ugani maeneo ya Mijini. Kwanza tukiri kwamba Maafisa Mifugo wetu walioko katika Taifa letu wanahitajika mahali pote kwa sababu hata huko Mjini ambapo Mheshimiwa Mbunge anapasema pia kuna wafugaji. Kama si wafugaji wa kufuga ng’ombe wa kuchunga kama vijijini wako wafugaji wanafuga ndani kwa ajili ya kuzalisha maziwa. Kwa hiyo Maafisa Ugani tukubali kwamba wanahitajika maeneo yote.
Mheshimiwa Spika, issue hapa ni upungufu wa Maafisa Ugani tulionao katika nchi yetu, hii inatokana na uwezo wa kifedha wa kibajeti ambao kama tungepata fedha za kutosha maana yake tungekuwa tunaajiri Maafisa Ugani wa kutosha katika Taifa letu, mijini na vijijini kwa sababu kote panahitaji Maafisa Ugani.
Mheshimiwa Spika, hili la pili kuhusu tozo. Sisi Wizara ya Mifugo hatuna tozo nyingi kiasi hicho. Tozo nyingi ziko katika Halmashauri ambako Mheshimiwa Mbunge ni Mjumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango, nafikiri kule wakikaa kwenye vikao vyao sasa waende kupunguza tozo kwa wafugaji wetu ili wafugaji wetu waweze kufuga ufugaji watija.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved