Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ally Anyigulile Jumbe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Primary Question
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza:- Je, vikwazo gani vinasababisha Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kyela usipandishwe hadhi kuwa Halmashauri ya Mji?
Supplementary Question 1
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, mamlaka hii ina zaidi ya miaka 16 na leo hapa tunapata majibu ambayo ni too general na hayaoneshi matumaini ya kwamba ni lini sasa mamlaka hii itapandishwa. Nina maswali mawili. Swali la kwanza; madiwani zaidi ya 14 hawana KAMAKA (Kamati za Maendeleo) wanaelea na kumeingia mgogoro wa maslahi ambapo Wenyeviti wa Vitongoji na Madiwani hawawezi kukaa pamoja kirahisi na kufanya maendeleo, je, Serikali inafikiria nini kwenye jambo kama hili?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Halmashauri ya Wilaya ya Kyela inaendesha mabaraza mawili kwa wakati mmoja, Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo na Baraza la Halmashauri ya Madiwani pale Kyela. Je, Serikali haioni ni wakati sahihi kuzisaidia pesa halmashauri zilizo katika hali hiyo ili ziweze kuendesha hayo mabaraza mawili kwa wakati mmoja? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali inatambua uwepo wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kyela kwa kipindi cha takribani miaka 16. Kwa kipindi hicho chote mamlaka ile haijawahi kukidhi vigezo vya kuwa halmashauri ya mji ikiwemo idadi ya wananchi, ukubwa wa kijiografia wa eneo husika pamoja na vigezo vingine. Walishawahi kuleta maombi hayo, Serikali ilifanya tathmini na kuwapa maelekezo ya kwenda kufanya maboresho. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mbunge kwamba tunahitaji kupata halmashauri ya mji lakini tunasubiri kwanza vigezo viweze kutimia. Ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, suala la pili, tunaelekeza Wenyeviti na Madiwani wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kyela na Baraza la Madiwani, waweze kufanya kazi kwa ushirikiano na ni kazi ya Mkurugenzi na Viongozi wote wa Serikali kuhakikisha kwamba wataalam hawa, watendaji hawa na viongozi hawa wa vijiji na kata wanafanya kazi kwa ushirikiano.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusiana na Serikali kupeleka fedha za ziada kwa ajili ya kuendesha Baraza la Mamlaka Mji Mdogo na Baraza la Madiwani. Suala hilo linatokana na mapato ya ndani ya halmashauri. Kwa hiyo, nisisitize kwamba Halmashauri ya Kyela kupitia mapato ya ndani waendelee kuhudumia pia Mamlaka ya Mji Mdogo mpaka pale mamlaka hiyo itakapopandishwa hadhi au itakapoondolewa kwenye orodha ya Mamlaka za Mji Mdogo.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved