Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joseph Michael Mkundi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Primary Question
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:- Je, kwa nini ujenzi wa Barabara ya Bukiko hadi Bwisya kupitia Katende inayosimamiwa na TARURA haukamiliki kwa zaidi ya miaka miwili sasa?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kutambua changamoto za kijiografia ambazo zimekuwa zinaathiri utendaji na kupata wakandarasi bora kwenye maeneo ya pembezoni kama Ukerewe, mwaka jana Serikali iliniahidi kutupatia vifaa vya ujenzi kama magreda na kadhalika kwa ajili ya kuondoa changamoto hiyo. Nataka kujua na Wakerewe wanataka kujua hatua ipi imefikiwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa pesa za mafuta kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji kwa TARURA zinapelekwa mkoani jambo ambalo limekuwa linaathiri wahandisi wilayani kufuatilia hasa inapotokea dharura. Ni upi sasa mkakati wa Serikali kufanya marekebisho ya utaratibu huu? Nashukuru sana. (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ilitoa ahadi ya kupeleka magreda na vifaa mbalimbali vya ujenzi wa miundombinu ya barabara na ahadi hii mpaka sasa bado haijatekelezwa. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua umuhimu wa upatikanaji wa vifaa hivi katika jimbo lake na inafanya taratibu za upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kununua vifaa hivyo ili viweze kupelekwa. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itatekeleza ahadi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, Serikali inatambua changamoto aliyoiainisha Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na upatikanaji wa fedha kwa wakati kwa ajili ya TARURA kuweza kutoa huduma zake kwa dharura. Kwa muktadha wa suala hili analozungumza Mheshimiwa Mbunge, Serikali itaendelea kuhakikisha inasimamia upatikanaji wa fedha za TARURA kutoka Serikali Kuu lakini kutoka katika Serikali ya Mkoa zinapatikana kwa wakati ili kuweza kutimiza mahitaji ya ujenzi wa barabara kwa dharura. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved