Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Doto Mashaka Biteko
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukombe
Primary Question
MHE. DOTO M. BITEKO aliuliza:- Maafisa wa Idara ya Misitu walivamia wananchi wa kitongoji cha Idosero kilichosajiliwa kwa GN na kuchoma nyumba 40 za wananchi na kuharibu mazao yao. Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Idosero kwa hasara kubwa waliyopata?
Supplementary Question 1
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naomba nimshukuru sana Naibu Waziri kwa ushirikiano anaonipa kila wakati napoenda kumuona kwa mambo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimpe taarifa kidogo Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba lile zoezi la kuondoa wananchi kwenye msitu ule kama anavyosema kwamba walishirikisha Halmashauri si kweli nadhani kuna mahali fulani aliyempa taarifa hakusema ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya ya Bukombe eneo lake kubwa ni hifadhi na wananchi wanafuata huduma za maliasili Wilayani Kahama umbali wa kilometa zaidi ya 96. Je, Serikali haioni kuwa sasa muda umefika ifungue Ofisi ya Maliasili Wilayani Bukombe ili wananchi wanaofanya shughuli mbalimbali kama za kurina asali vibali vyao sasa wasihangaike kufuata Kahama ambako ni mbali sana?
Swali la pili, jambo lililotokea au tukio lililotokea Idosero linatishia vilevile vijiji mbalimbali ambavyo viko jirani, vijiji kama vile Nyakayondwa, Pembe la Ng’ombe, Kichangani, Matabe, Mwabasabi, Ilyamchele ambavyo viko Wilayani Chato vinatishiwa na jambo hili. Lakini vilevile kijiji kama vile Nyamagana, Ilyamchele vilivyoko kata ya Namonge, Wilaya Bukombe na vyenyewe wananchi wake hawajakaa kwa utulivu kwa sababu ya matishio haya haya. Serikali inawaambia nini wananchi hawa ili waweze kuishi kwa amani? Nakushukuru.
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la umbali kutoka Kahama mahali ambapo wananchi hawa wa Bukombe wanakwenda kupata huduma zinazohusiana na masuala ya maliasili na ombi lake la kuletwa kwa kituo mahususi kwenye eneo la Bukombe au kwenye Wilaya ya Bukombe ili kuweza kurahisisha utekelezaji wa shughuli za maliasili, napenda tu kwanza nimhakikishie kwamba nia njema inaonyesha wazi kwamba si kuleta huduma tu peke yake bali pia hata kuiwezesha Wizara ya Maliasili na Utalii kuweza kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa sheria inayohusiana na suala la uhifadhi. Kwa hiyo, hilo ni jambo jema na ninalichukua na tunalipokea na tutalifanyia kazi ili kuweza kuona ni namna gani tunaweza kupata kituo kwenye eneo ambalo liko karibu na litakalowezesha wananchi kuweza kufika kwa karibu kutoka kwenye Wilaya ya Bukombe.
Kuhusu suala la vijiji jirani ambavyo vinaonekana kuwa na changamoto zinazofanana na zile tulizokutana nazo Idosero kwanza kwa kutamka tu kwamba ni vijiji maana yake ni kwamba ni vijiji vinavyotambuliwa kisheria na Serikali. Ukisema vijiji maana yake ni vijiji vya mujibu wa sheria na vimesajiliwa kwa hiyo, sasa kama nilivyotangulia kusema kwa upande wa Idosero. Kwamba kwa kuwa Idosero kama kitongoji ilipata GN chini ya Sheria ya Serikali na vilevile vijiji vilivyotajwa vilevile kwa kuwa ni vijiji uwepo ni kwa mujibu wa sheria basi nimesema sasa umefika wakati wa kwenda kuangalia sheria zote; hii ya maliasili na utalii na ile iliyoanzisha hivyo vijiji twende kuona namna gani tunaweza tuka-harmonize tuweze kupata suruhisho la kudumu, badala ya hizi operations ambazo zinazofanyika mara kwa mara na hazina majibu ya kudumu.
Name
Kangi Alphaxard Lugola
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwibara
Primary Question
MHE. DOTO M. BITEKO aliuliza:- Maafisa wa Idara ya Misitu walivamia wananchi wa kitongoji cha Idosero kilichosajiliwa kwa GN na kuchoma nyumba 40 za wananchi na kuharibu mazao yao. Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Idosero kwa hasara kubwa waliyopata?
Supplementary Question 2
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona kwa kuwa kwenye swali la msingi la Mheshimiwa Doto inaonyesha Wizara ina nguvu za kutosha za kupambana na wananchi ambao wanavamia maeneo ya hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini sasa Wizara ya Maliasili itatmia nguvu hizo hizo kuzielekeza kwenye Ziwa Victoria kupambana na mamba ambao pia wamevamia wananchi wangu kuwala na wengine kuwajeuri ili kuhakikisha kwamba wanawavuna wasiendelee kuleta madhara kwa wananchi wa Mwibara?
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza si sahihi sana kusema kwamba Serikali inatumia nguvu nyingi sana kwa maana ya matumizi ya mabavu wakati wa kusimamia sheria zake. Inawezekana hapa na pale watekelezaji wa sheria pengine huweza kufanya yale ambayo si sahihi sana. Lakini jambo la msingi sana kwa upande wa Serikali ni kusimamia sheria kwanza kwa kutoa elimu kuwaelimisha wananchi ili wasiweze kukiuka sheria na kuweza kutii sheria kwa hiyari huo ndiyo mwelekeo.
Lakini kuhusu suala la mamba wanaosumbua pengine wanaleta madhara ya wananchi kuuawa au kujeruhiwa hili ni suala ambalo limo pia kwa mujibu wa kanuni na taratibu upo utaratibu wa kufanya uvunaji kwa utaratibu ambao unatambulika kisheria na kisayansi na pale ambapo inaonekana kuna haja ya kuchukua hatua ambazo ni za dharura zaidi kuliko ule utaratibu wa uvunaji, basi utaratibu huo unaweza ukafuatwa. Sasa kwa kuwa ametaja eneo mahususi kule Ukerewe nalichukua na naliorodhesha na tutaenda kuangalia ni kwa kiwango tatizo hili la mamba linaleta matatizo kwenye eneo alilolitaja ili tuweze kuona kama tunatumia kanuni za kawaida za uvunaji ama tunaweza kulichukua kama suala la dharura na kuweza kwenda kuchukua hatua zinazostahili.
Name
Mohamed Omary Mchengerwa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rufiji
Primary Question
MHE. DOTO M. BITEKO aliuliza:- Maafisa wa Idara ya Misitu walivamia wananchi wa kitongoji cha Idosero kilichosajiliwa kwa GN na kuchoma nyumba 40 za wananchi na kuharibu mazao yao. Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Idosero kwa hasara kubwa waliyopata?
Supplementary Question 3
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru huku nyuma hatuonekani inatubidi tuanze kunywa maji ya kutosha.
Swali langu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, Rufiji tunabeba asilimia 49.8 la eneo la hifadhi na misitu nikimaanisha square kilometer 6,300 ziko ndani ya hifadhi na misitu, na kati ya hizo square kilomita 13,000 ndiyo eneo kubwa la Jimbo langu la Rufiji. Wananchi wa Jimbo la Rufiji wana masikitiko makubwa katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii ambapo hatujaingiwa katika mgao wa madawati.
Waziri, umetumia kigezo gani kugawa madawati katika maeneo ambayo wanatunza hifadhi ya misitu yetu naomba kufahamu hilo kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Rufiji?
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani inawezekana anazungumzia suala la mgao wa madawati uliofanywa hivi karibuni na Wizara kupitia TANAPA na kama hivyo ndivyo ningependa tu nimueleweshe tu kwamba TANAPA ni wasimamizi au wanashughulikia masuala ya uhifadhi, lakini kwenye hifadhi za wanyamapori siyo misitu. Na kigezo kilichotumika kwa kipaumbele ni kuangalia cha kwanza kuangalia maeneo yanayopakana na hifadhi hizo za wanyamapori tena zile ambazo ziko chini ya TANAPA hilo ni kuhusu swali hilo la mgao wa juzi. Lakini kwa upana wake ni kwamba kila wakati tutakapokwenda kuangalia sasa namna ambavyo jamii zinazoishi jirani na maeneo ya hifadhi au ya wanyamapori ni ilani ya Chama cha Mapinduzi, ni content ya ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba hawa wanaoishi jirani ndiyo wawe wanufaika wa kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama kwenye eneo hili la misitu anakokuzungumzia kule Rufiji hali ilivyo ni hivyo alivyosema basi nakwenda kutizama kama hivi karibu tumefanya uvunaji wa aina yoyote au kama hivi karibuni limejitokeza jambo lolote ambalo lina maslahi kwa wananchi niende kuangalia kama kulitokea kasoro ya kuweza kutowahusisha wananchi ambao amewazungumzia kwenye eneo lake. Na ikiwa hivyo ndivyo basi Serikali itachukua hatua za mara moja kurekebisha.