Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dennis Lazaro Londo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mikumi
Primary Question
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutunza mazingira ya Bwawa la Zombo Kilosa ili litumike kwa shughuli za ufugaji wa samaki na kilimo?
Supplementary Question 1
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, bwawa hili limekosa matunzo na hivyo kina chake kimezidi kupungua siku baada ya siku na kusababisha mafuriko katika maeneo ya Miombo, Masanze na Kijiji cha Changarawe.
Je, Serikali ina mpango gani kuokoa maisha ya wananchi hawa kutokana na kadhia ya mafuriko ambayo inatokana na bwawa hili kukosa matunzo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya kutoka Mikumi kwenda Kilosa ndani ya kipindi hiki cha mvua imekatika mara nne na kukosa mawasiliano kabisa kati ya maeneo haya mawili kutokana na mafuriko yanayosababishwa na bwawa hili.
Je, Serikali haioni sasa wakati umefika Ofisi ya Makamu wa Rais kukaa na Wizara ya Ujenzi na Wizara ya kilimo ili kuona namna bora ya kudhibiti mafuriko haya ambayo yanasababishwa na shughuli zisizo endelevu katika Bwawa hili la Zombo maarufu kama Bwawa la Nara?
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lazaro Londo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii nimshukuru sana na kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwasemea wananchi kwenye jambo hili la mabwawa na mambo mengine ya uhifadhi wa mazingira.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mabwawa mengi hasa kipindi cha mvua yamekuwa yakifurika, yanajaa na ni kweli tumeona mabwawa mengi ambayo tuliyachimba sisi ama yalichimbwa na Wizara nyingine ama taasisi nyingine yamekuwa hayapo kama yalivyokuwa zamani yakiwepo na changamoto za uingiaji wa michanga. Tulichogundua ni kwamba michanga hii inaingia, kwanza ni kwa sababu za shughuli za kibinadamu zinazofanyika zikiwemo shughuli za ufugaji, shughuli za makazi, lakini hata shughuli za kilimo. Kuna watu wanalima karibu na maeneo haya basi michanga inaingia humo mwisho wa siku mabwawa yanafurika halafu yanakuja kuleta shida kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, nimwambie tu Mheshimiwa kwamba Serikali tunakwenda kutafuta fedha za kuona namna ambavyo tunaweza tukatoa michanga, lakini pia kuweza kutoa takataka nyingine ambazo zipo ndani ya mabwawa haya ili kuweza kusafisha na yasiweze kuleta athari.
Mheshimiwa Spika, aidha tunakwenda kushirikiana na Wizara nyingine ikiwemo Wizara ya Kilimo kwa sababu shughuli hizi za uchimbaji zinafanyika, kwa hiyo tutakwenda kushirikiana na Wizara nyingine.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala hili la barabara nimwambie Mheshimiwa tuko tayari kushirikiana na Wizara nyingine ili kuokoa mabwawa haya ili yasijae maji yakafunga barabara au njia yakaleta athari kwa wananchi, nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved