Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. MWITA M. WAITARA K.n.y. MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, ni lini Serikali italipa fidia au kurejesha maeneo ya wananchi katika Mlima Nkongore yaliyochukuliwa na Jeshi la Magereza – Tarime?

Supplementary Question 1

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, eneo hili Mheshimiwa Michael Kembaki, ameuliza mara kadhaa huku Bungeni, amemchukua Mheshimiwa Diwani wa Kata husika yeye mwenyewe wamekaa kikao cha wilaya na mkoa wakakubalina eneo hilo lisirudishwe kwa wananchi, lakini lirudishwe kwa jamii ile nalipangiwe matumizi ya kijamii, tuna uhaba mkubwa wa ardhi. Je, yamkini inaonekana Wizara ya Mambo ya Ndani ndio kikwazo na ndio wanazuia huo mpango usitekelezwe. Nataka nijue sababu ya Wizara kukataa ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kule Tarime Vijijini eneo la Mwema na Kata ya Regicheri, eneo lingine wamechukua wakawapa JKT wanalima, halafu lingine wamezuia zaidi ya mwaka mzima hakuna shughuli inafanyika pale. Je, huu utaratibu wa kutwaa maeneo ya watu wa Tarime na kuyahodhi na watu wanakuwa na shida ya kilimo utaisha lini? (Makofi)

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Waitara, kwa niaba ya Mheshimiwa Kembaki, naomba kujibu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mlima huu kurudishwa kwa jamii badala ya kusimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, nimeeleza msingi wa uamuzi ule ilikuwa moja, ni kuhifadhi mlima ule, lakini pili ni kuzuia uharamu wa mazao yaliyokuwa yanalimwa kwenye eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Mbunge alikuja sasa sijui alikutana na nani waliopatana, lakini kwa msimamo wa Wizara na kwa msimamo wa Kamati ya Usalama ya Wilaya eneo lile lipo nchi ya uangalizi wa Magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la pili, la Mheshimiwa Waitara, naona ni kama amechomekea Mambo ya Ndani, kama ni JKT basi ni la Wizara ya Ulinzi, nimshauri aandae swali la msingi ili liweze kujibiwa ipasavyo na Wizara yenye dhamana na ulinzi, ahsante. (Makofi)

Name

Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWITA M. WAITARA K.n.y. MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, ni lini Serikali italipa fidia au kurejesha maeneo ya wananchi katika Mlima Nkongore yaliyochukuliwa na Jeshi la Magereza – Tarime?

Supplementary Question 2

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa magereza mengi yana mwonekano wa kuchoka sana, kwa mfano Gereza la Mjini Lushoto.

Je, ni lini Serikali itafanya utaratibu wa kuyakarabati magereza yote yakawa na sura ya matumaini ndani na nje haidhuru kwa kuwatumia wafungwa hao hao kwa kufanya kazi za ujenzi? (Makofi)

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi lilikuwa kutwaa eneo na kutumiwa na magereza, lakini ninaweza nikamjibu kwa sababu nina background kidogo ya eneo hilo. Ninafahamu mpango wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kujenga upya magereza kwenye maeneo ambayo hayana magereza, lakini pia kukarabati magereza ambayo yamechakaa na ukarabati huo umeenza katika maeneo mbalimbali ili kuboresha hali ya magereza hizo.

Kwa hiyo, nimpe uhakika Mheshimiwa Mbunge kwamba kadiri hali ya fedha itakavyoruhusu kwa maana ya bajeti magereza kama alivyorejea hilo la Lushoto, litakarabatiwa ili lilingane na hadhi kama ambavyo ameshauri, nashukuru.

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWITA M. WAITARA K.n.y. MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, ni lini Serikali italipa fidia au kurejesha maeneo ya wananchi katika Mlima Nkongore yaliyochukuliwa na Jeshi la Magereza – Tarime?

Supplementary Question 3

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nisikitike kwa majibu ya Serikali, baada ya ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ambaye ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa Wilaya, walikaa na wakakiri kwamba watalirejesha lile eneo kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwa kwa majibu uliyotoa hapa eneo lilochukuliwa ni zaidi ya eka 100 na imeathiri zaidi ya kaya 67 na kwa kuwa magereza wanafanya shughuli za kilimo kwenye hilo eneo. Serikali haioni sasa kuna haja ya kupeleka Mradi wa BBT ili wananchi wa eneo lile waendelee kufanya shughuli zao za kilimo na kupata kipato? (Makofi)

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua umuhimu wa wananchi kuwa na ardhi ya kutosha kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameshauri, lakini kwa sababu uamuzi ulishafanyika na kwa sababu ya ujirani mwema pengine kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nchi, nishauri kwamba uongozi wa Magereza Mkoa wa Mara, uwasiliane na utawala ngazi ya Halmashauri ya Mji wa Tarime ili kuona namna ambavyo kwa ujirani mwema wanaweza wakaishi kati ya magereza na wananchi ambao wanahitaji eneo kwa ajili ya hicho kilimo, nashukuru.