Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Josephat Mathias Gwajima
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kawe
Primary Question
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: - Je, lini Serikali itakuja na mkakati wa kutumia gesi asilia kuendesha magari nchini ili kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta nje ya nchi?
Supplementary Question 1
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Serikali nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hii gesi asilia (CNG) sasa inatumika kwenye gari nyingi, je, hamuoni kuwa sasa ni wakati mwafaka wa kufungua vituo njiani ili mtu anapokuwa anasafiri kutoka Dar es Salaam kuja hapa kuwe na vituo maalumu kabisa vya gesi asilia ambako mtu anaweza kujaza kwenye gari lake?
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Askofu Josephat Gwajima. Ni kweli kwamba Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi tumeanza mkakati wa kutafuta namna ya kuwa na vituo kwa gari binafsi kuanzia Dar es Salaam mpaka Dodoma kwa awamu ya kwanza. Tayari tumekwishaanza kuwa na mkakati huo na tayari wadau wa sekta binafsi wameshaanza kujitokeza kwa ajili ya kuwekeza kwenye ujenzi wa vituo barabarani kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma. Hata kwa upande wa magari ya Serikali tayari TPDC imeanza kuongea na Bohari za GPSA ili kuongeza vituo vya CNG kwenye hivi vituo vya bohari kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ili pia hata magari ya Serikali nayo yakiwa yamekwishabadilishwa yaweze kujazwa gesi kutokea Dar es Salaam – Dodoma ambapo ndiyo njia kuu ya magari haya kwa kiasi kikubwa yanapopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa kwa pande zote mbili za magari binafsi pamoja na magari ya Serikali tumekwishaanza kulifanyia kazi suala hili ili kuongeza idadi ya magari ambayo yanatumia CNG, ahsante.
Name
Munira Mustafa Khatib
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: - Je, lini Serikali itakuja na mkakati wa kutumia gesi asilia kuendesha magari nchini ili kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta nje ya nchi?
Supplementary Question 2
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kuwa Serikali ina mpango kuwa ifikapo mwaka 2030/2034 wananchi wote wawe wanatumia nishati safi na salama.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wanasambaza mabomba kwenye nyumba ili ifikapo mwaka 2030/2034 wananchi wote wawe wanatumia nishati safi na salama? (Makofi)
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, na nimshukuru Mheshimiwa Munira kwa swali zuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali tulikwishaanza awamu ya kwanza ya majaribio kwa ajili ya kuweka miundombinu kwenye maeneo ya Mikocheni pamoja na Mbezi. Aidha, kwa sasa tayari tumeanza mchakato wa kuendelea kuwekeza katika miundombinu hii kwa maeneo mengi zaidi hususan kwa Mkoa wa Dar es Salaam kwanza ili wananchi wengi waweze kutumia gesi nyumbani, kwa sababu ni ukweli kwamba gesi ya nyumbani kwa miundombinu ina bei nafuu kuliko ile ya mitungi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tayari mikakati ipo ya kuendelea kuongeza miundombinu nyumbani ili wananchi wengi waweze kutumia gesi nyumbani na tufikie azma ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha 80% ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. (Makofi)
Name
Tarimba Gulam Abbas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Primary Question
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: - Je, lini Serikali itakuja na mkakati wa kutumia gesi asilia kuendesha magari nchini ili kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta nje ya nchi?
Supplementary Question 3
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa juhudi zake za kuleta teknolojia ya gesi katika gari, lakini sasa hivi teknolojia imepanda sana kiasi kwamba kuna magari ya kutumia umeme.
Je, Serikali ina juhudi gani katika kuangalia vilevile uwezekano wa kuhamasisha kuleta magari ya umeme nchini ili kuendelea kupunguza matumizi ya mafuta na gesi?
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nishukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inaangalia njia mbalimbali kwa ajili ya kuhamasisha matumizi mbadala, kwa sababu tunaamini ajenda zote hizi zinalenga kwenye kuongeza jitihada za kupambania suala la mazingira. Kwa hiyo, kama ambavyo tunawekeza kwenye nishati ya gesi kwenye magari ndivyo ambavyo tumeshaanza mikakati ya kuweka pia mazingira wezeshi kwa ajili ya kuleta magari yanayotumia umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge jambo hili pia Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kuanzia mwaka jana alishalianza na sisi tunaendelea nalo ili kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira wezeshi kwa ajili ya matumizi ya magari ya umeme, ahsante.
Name
Mohammed Said Issa
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Konde
Primary Question
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: - Je, lini Serikali itakuja na mkakati wa kutumia gesi asilia kuendesha magari nchini ili kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta nje ya nchi?
Supplementary Question 4
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, hapa katika majibu yake ya msingi Mheshimiwa Naibu Waziri anasema Serikali inahamasisha kwa kupunguza kodi magari ambayo yanatumia gesi, lakini magari yaliyopo nchini ni mengi sana na yanahitaji kutumia gesi. Gharama za ku-install mitambo ya gesi kwenye magari ni kubwa sana, ni takribani shilingi milioni 2.5. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba gharama hizi zinashuka?
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nishukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama hizi ziko juu kidogo ndiyo maana Serikali tumeendelea kuhamasisha watu wengi zaidi na kampuni nyingi zaidi ziweze kuwekeza katika kuwa na karakana. Tunakubali mwanzo huwa ni mgumu sana, lakini tunakoelekea ni kuzuri kuliko tulikotoka. Mwaka 2021 wakati tunaanza kuhamasisha matumizi ya gesi kwenye magari, kwa wastani tulikuwa tuna-convert takribani magari 1,159, leo tunavyoongea tuna magari 5,100 katika mwaka huu wa 2022/2023. Hii ni kwa sababu karakana zimeongezeka kutoka ile moja ya DIT hadi nane. Kwa hiyo, wawekezaji wengi wanavyokuja ndivyo ambavyo gharama inavyoendelea kushuka kutokana na ushindani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tunaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza zaidi na kuja na teknolojia bora zaidi. Tukiwa na karakana nyingi zenye teknolojia ambayo ni bora gharama zitapungua. Kwa hiyo, tunaendelea kulifanyia kazi ili kuhakikisha kuwa gharama hizi zinapungua, ahsante.
Name
Rehema Juma Migilla
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Primary Question
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: - Je, lini Serikali itakuja na mkakati wa kutumia gesi asilia kuendesha magari nchini ili kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta nje ya nchi?
Supplementary Question 5
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na kwanza tuipongeze Serikali kwa kuanzisha hii teknolojia ya kutumia gesi kwenye magari yetu, lakini magari mengi yanayotumia hii gesi ni magari ya petroli tu.
Je, Serikali ina mpango upi wa kuhakikisha kwamba magari yanayotumia dizeli nayo yaanze kutumia gesi kwani tunaona Kampuni ya Dangote magari yake yanatumia dizeli, lakini wamefanya installation ya mitungi ya gesi, mpango ni upi?
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tumeanza programu hizi na kwa sasa hivi tulikuwa tuna vituo vitano tu, lakini ili kuelekea kuwa na vituo vingi zaidi tumeanza mazungumzo na hao wawekezaji wa kwenye sekta binafsi ili kuhakikisha wanaona namna ya kuwa na mifumo yote miwili, yaani petroli pamoja na dizeli. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tunaendelea kulifanyia kazi ili kupata namna ya kuyafanya magari yanayotumia dizeli nayo kuweza kubadilishwa mfumo.