Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Innocent Sebba Bilakwate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyerwa

Primary Question

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA Wilayani Kyerwa?

Supplementary Question 1

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na kwanza niishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wana-Kyerwa wanapenda kufahamu fedha imetengwa tangu mwaka 2022/2023 lakini mpaka sasa hivi ujenzi unaenda kwa kusuasua. Tungependa kujua je, ni kwa nini? (Makofi)

Swali la pili, kwa kuwa vifaa vinatoka kwenye Wizara na hii inaweza ikawa sababu ya kuchelesha ujenzi huu, je, kwa nini fedha yote isipelekwe kwenye halmashauri ili ujenzi usimamiwe na halmashauri kama ilivyo miradi mingine kama hospitali za wilaya na vituo vya afya? Ahsante.

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, amekuwa akifuatilia ujenzi wa chuo hiki kwa muda mrefu na hata pale Serikali tulipokuwa hatujaanza ujenzi alifuatilia kuhakikisha kwamba chuo hiki kinajengwa kwenye eneo lake, lakini hata tulipoanza ujenzi mwishoni mwa mwaka 2022. Ujenzi huu ulianza mwezi Juni, 2022 ambapo ni mwishoni kabisa mwa mwaka wa fedha, alifuatilia mwenendo pamoja na maendeleo ya ujenzi huu. Kwa hiyo, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa ajili ya ufuatiliaji huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jambo lake la kwanza kuhusiana na suala la ujenzi kusuasua, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, ni kweli Serikali ilitenga fedha na fedha hii ipo ingawa tunapeleka kule fedha hii kwa awamu. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba kuna vifaa vile ambavyo tunasema ni local materials ndizo hizi ambazo ni shilingi milioni 324 zimepelekwa kule kwa ajili ya ununuzi wa mchanga, maji, mawe na kulipa mafundi ambao wanahudumia kwenye hili eneo letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ujenzi huu haujasuasua sana, lakini tunajua kwamba unakwenda taratibu kutokana na ufuatiliaji wa karibu na kuhakikisha kwamba kila kitu kinakwenda sawasawa. Kwa vile ametupa kama ushauri tutahakikisha katika kipindi hiki kifupi tuharakishe ujenzi ule ili Wana-Kyerwa nao waweze kupata chuo hiki kwa ajili ya mafunzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo lake la pili la vifaa kwamba tupeleke kule fedha kule kwa ajili ya vifaa. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu, kwa nini tumeamua kununua vifaa hivi kwa kutumia utaratibu wa ununuzi wa pamoja au bulk purchase?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ununuzi wa pamoja (bulk purchase) tumepata faida nyingi sana. Kwanza tumetengeneza exemption ya zile kodi kwenye upande wa nondo, cement na vifaa vyote vile ambavyo vinatoka viwandani. Kwa hiyo, eneo lile ambalo tulipata exemption limetusaidia kwenda kufanya kazi zaidi ya pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wake huu wa kusema tupeleke fedha kule, tutapeleka fedha zile za local materials, lakini fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya viwandani tunadhani ni bora tununue moja kwa moja kwa sababu ina manufaa makubwa kuliko tungepeleka fedha hizi zote kule, matumizi yake yangekuwa makubwa na ile value for money tungeweza kuikosa, nakushukuru sana.

Name

Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Primary Question

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA Wilayani Kyerwa?

Supplementary Question 2

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Halmashauri ya Ushetu tayari imekwishatenga eneo zaidi ya hekari 42 na lina hati na kila kitu, je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa shule hii ya ufundi katika Halmashauri ya Ushetu?

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali dogo la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Cherehani kwa kutenga eneo lile la Ushetu kwa ajili ya ujenzi wa shule zile za ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilikuwa najibu swali hapa, azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba yale majimbo ambayo hatujajenga Chuo cha VETA tutakwenda kujenga shule ya ufundi. Kazi hii tunatarajia ianze mwaka ujao wa fedha wa 2024/2025. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Cherehani na wananchi wa Ushetu, Serikali ya Mama Samia iko kazini na mwezi Julai mwaka ujao wa fedha shule zile 100 za elimu ya amali tutakwenda kuanza ujenzi wake likiwemo na eneo la Ushetu.

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA Wilayani Kyerwa?

Supplementary Question 3

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, Wilaya ya Tarime ina halmashauri mbili, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Halmashauri ya Mji wa Tarime. Halmashauri ya Wilaya ya Tarime tumepata Chuo cha VETA, lakini Halmashauri ya Mji wa Tarime ambayo ni makao makuu ya wilaya hatujapata. Nataka kujua umesema hapo ujenzi wa shule za ufundi utaanza Julai, je, Halmashauri ya Mji wa Tarime nayo inaenda kujengewa hiyo shule ya ufundi?

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Matiko, kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Matiko kwa ufuatiliaji wa karibu kuhusiana na masuala ya elimu na taaluma kwenye mkoa wake pamoja na wilaya zake zote za Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Matiko, azma ya Serikali ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga Vyuo vya VETA katika wilaya, tunafahamu kwamba kuna wilaya ambazo ni kubwa na zina majimbo zaidi ya moja. Kwa hiyo, kwenye maeneo yote au wilaya zote ambazo zina majimbo zaidi ya moja, tunaangalia ni eneo gani au jimbo gani limejengwa Chuo cha VETA. Kule ambako hakujajengwa Chuo cha VETA azma ya Serikali ni kupeleka shule ya amali au hizi shule za ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili Jimbo la Tarime Mji lina shule ya ufundi na ni miongoni mwa wilaya au majimbo ambayo ujenzi utaanza mwaka ujao wa fedha, ninashukuru sana.