Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rehema Juma Migilla
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Primary Question
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa bwawa katika Kijiji cha Ichemba?
Supplementary Question 1
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu haya yanakatisha tamaa kabisa hasa kwa wananchi wangu ambao wana ndoto kabisa za kutumia hili bwawa, lakini sambamba na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa bwawa hili umekuwa kwenye Ilani ya Uchaguzi kwa awamu mbili mfululizo mwaka 2015 mpaka 2020 limo ikapita bila, lakini mwaka 2020 mpaka mwaka 2025 bwawa hili na lenyewe limo. Ujenzi wa bwawa hili ukikamilika utakwenda kuzisaidia kata zangu tisa na vijiji 27 lakini cha ajabu mpaka leo hivi tunavyoongea hakuna shughuli yoyote iliyoanza kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo.
Je, hatuoni kwamba kucheleweshwa kwa ujenzi wa bwawa hili siyo tu kwamba unamchonganisha Mheshimiwa Rais na wananchi, lakini pia unaniletea mimi ajali kwa wananchi wangu kwamba siwajibiki kwao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, tumeona miradi mingi ya ujenzi wa maendeleo inapofanyika, wale wananchi wanaozunguka maeneo hayo hulipwa fidia, lakini cha ajabu wananchi wanaozunguka mradi wa hili bwawa hawajafanyiwa hata tathimini juu ya kulipwa fidia au kifuta jasho.
Je, ni upi mpango wa Serikali ili kuwapa kifuta jasho au fidia wananchi hao ambao kwa ridhaa yao wameacha maeneo yao ambayo walikuwa wanafanyia shughuli zao za kimaendeleo ili kuacha mradi ufanyike, upi ni mpango?
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, jambo la kwanza nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali haiko hapa kukatisha tamaa wananchi na wala wewe Mbunge kukutengenezea ajali kwa wananchi wako, hiyo siyo wajibu wa Serikali. Jukumu letu sisi kama Serikali ni kuhakikisha tunatatua changamoto kwa wananchi hususani kwenye hili eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelitaja la ujenzi wa bwawa, bwawa hili tunajenga kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tulishakubaliana kwamba katika eneo lolote ambalo tunajenga bwawa ni lazima Wizara tatu tuhusike ikiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa maana ya kusaidia wananchi wale hususani wafugaji pamoja na kufuga samaki katika maeneo yale. Kwa hiyo, hizi kazi tunafanya kwa pamoja na ndiyo maana unaweza kuona limechukua muda mrefu kidogo kwa sababu ni lazima lizingatie Wizara zote tatu katika ujenzi wa aina moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana katika hatua za sasa Wizara ya Maji wako katika hatua za mwisho ili waweze kuja kumtangaza mkandarasi ambaye ataanza ujenzi na sisi Wizara ya Kilimo tutachukua jukumu la kutoa maji katika bwawa na kutengeneza zile irrigation schemes kwenda kwenye mashamba ya wananchi, huo ndiyo wajibu wetu ambao sasa hivi tuko katika hiyo hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la fidia hakuna jambo lolote ambalo Serikali tutafanya bila kuzingatia maslahi ya wananchi wa eneo husika.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved