Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Bupe Nelson Mwakang'ata
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji uliopo Mpasa, King’ombe, Kata ya Kala, Wilayani Nkasi?
Supplementary Question 1
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na ninaipongeza, kama imemaliza kutengeneza mradi huo, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan amenunua magari/mitambo ya kuchimbia visima kila mkoa. Napenda kujua ni kwa nini sasa Mji Mdogo wa Namanyere bado hawajachimbiwa visima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Bwawa la Maji la Mji Mdogo wa Namanyere ni muhimu sana kwa Wilaya ya Nkasi. RUWASA wamejipangaje kumaliza ujenzi wa Bwawa la Maji la Mji Mdogo wa Namanyere? Ahsante.
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Rukwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, ameendelea kuwa msemaji mkuu wa wanawake wa Mkoa wa Rukwa kuhusiana na suala la maji, nakupongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa hili swali inawezekana likaulizwa na Waheshimiwa Wabunge wengi kuhusu mitambo ambayo Mheshimiwa Rais ameinunua. Mitambo hii iliponunuliwa ni kwamba hatukuwa tumejiandaa na wataalamu wa kuiendesha, matokeo yake mitambo hii imejikuta kwamba ikienda katika maeneo ya porini inakwama na wataalamu wetu wakawa bado hawajaiva kiutaalamu kiasi kwamba ikawa inaleta changamoto sana, lakini kwa sababu hiyo, Mheshimiwa Waziri, Juma Aweso, alielekeza wataalamu wetu wapatiwe mafunzo toshelezi ili waweze kuiendesha mitambo hii na kufanya kazi kwa ufanisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuhakikishia na Bunge lako Tukufu kwamba tayari Mheshimiwa Waziri ametoa mwongozo na kwa mwongozo huo sasa tunaenda kuanza uchimbaji wa visima kwa kutumia hii mitambo ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi sana kuinunua. Sasa inaenda kuanza kufanya kazi kwenye vile visima vitano vitano vya kila Mbunge ambavyo ni visima 900. Kwa hiyo, nakuhakikishia na Bunge lako kwamba mitambo hii sasa iko tayari kuingia kazini na kuweza kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusu Bwawa la Namanyere, Mheshimiwa Waziri ametoa maelekezo ya kutoa fedha takribani shilingi milioni 400 mwishoni mwa mwezi wa nne na tayari kweli, kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema zimeshatolewa na zimeshafika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaelekeza RUWASA kuhakikisha kwamba bwawa hili sasa linaanza kufanyiwa kazi kwa uharaka zaidi ili liweze kutoa mahitaji ambayo yametarajiwa na kutatua changamoto ya maji katika maeneo ya Namanyere, ahsante sana.
Name
Prof. Patrick Alois Ndakidemi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Primary Question
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji uliopo Mpasa, King’ombe, Kata ya Kala, Wilayani Nkasi?
Supplementary Question 2
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa furs ana naishukuru Serikali kwa shilingi milioni 500 ambazo zilikwenda kujenga mradi kwenye Kata ya Kimochi katika Vijiji vya Mdawi, Shia, Sango na Kisaseni, lakini havijapata maji. Je, Serikali ina mpango gani wa kutusaidia kupata maji katika vijiji hivi?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Serikali ilitenga shilingi milioni 500 na hasa katika bajeti hii ya mwaka 2024/2025 tumetenga fedha nyingine za kwenda kuhakikisha kwamba tunaenda kumalizia vijiji ambavyo vimebaki kufikishiwa huduma ya maji ambavyo ni Vijiji vya Sango, Mdawi pamoja na Shia. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwa sababu imekuwa ni ndoto yake kuhakikisha kwamba vijiji hivi vinapata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana.
Name
Aida Joseph Khenani
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Primary Question
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji uliopo Mpasa, King’ombe, Kata ya Kala, Wilayani Nkasi?
Supplementary Question 3
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Waziri hilo Bwawa la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Namanyere bajeti iliyotengwa ni shilingi bilioni 6.7, fedha iliyoenda ni shilingi milioni 950, leo tunazungumza ni tarehe 12 Juni, tunaenda kumaliza mwaka wa bajeti na mpaka sasa mkataba tu haujasainiwa. Ni upi mkakati wa Serikali ambao upo kuhakikisha hizi fedha zinakwenda na huu mradi unakamilika?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua changamoto ya bwawa hili na ninatambua kwamba wananchi wake wanasuburi kuona nini kinafanyika na kwa bahati nzuri pia Mheshimiwa Mbunge uliuliza kuhusu hili swali na nikakupa mkakati wa namna gani tunaenda kufanya. Naomba uwe na subira kwa sababu miradi hii inafanyika kwa hatua na mkandarasi akishapewa mkataba maana yake ni kwamba tutaanza kwa kumlipa advance, hatumlipi pesa yote, maana yake ni kwamba pesa nyingine itakayofuatia ni kulingana na ambavyo atakuwa ana raise certificate kulingana na progress ya kazi ambayo atakuwa anaifanya. Kwa hiyo, nakutoa wasiwasi, Serikali inatambua na tunaenda kulifanyia kazi kwa ukamilifu, ahsante sana.
Name
Kunti Yusuph Majala
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji uliopo Mpasa, King’ombe, Kata ya Kala, Wilayani Nkasi?
Supplementary Question 4
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Mheshimiwa Naibu Waziri ulifika Kata ya Soya, Kijiji cha Mbarada na ukakutana na wananchi na wakakueleza kilio chao cha uhaba wa maji, ukawaahidi upatikanaji wa maji haraka iwezekanavyo. Ni lini unapeleka mitambo hiyo Kijiji cha Mbarada ili waweze kupata maji safi na salama kwa wakati?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kunti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sikosei Kijiji cha Mbarada kiko Wilaya ya Chemba na katika maeneo ambayo tulisikitishwa sana kama Serikali, baada ya kukuta hali ya upatikanaji wa maji ambayo wanayatumia wananchi wa pale yalikuwa mabaya sana, lakini napenda nimpe taarifa kwamba baada ya ile ziara na mpaka sasa, tukimaliza kipindi cha Bunge hapa, naweza nikakuonesha mitambo imeshafika pale na maji tayari wameshaanza kuona namna ambavyo yanatoka. Tunaamini kwamba uchimbaji na usambazaji wa miradi ya maji una hatua, kwanza kupata chanzo, kutengeneza tenki, kujenga mtandao na baadae kutengeneza maeneo ya kuchotea maji. Kwa hiyo, mradi huu utakamilika na wananchi watapata huduma ya maji, ahsante sana.
Name
Jeremiah Mrimi Amsabi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Serengeti
Primary Question
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji uliopo Mpasa, King’ombe, Kata ya Kala, Wilayani Nkasi?
Supplementary Question 5
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, katika Wilaya ya Serengeti Miradi ya Maji ya Gesaria, Nyamitita, Rigicha na Nyiberekera imekwama kabisa. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa miradi hii?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Serengeti katika eneo la Nyamitita, tayari mkandarasi wetu yuko site, yuko kwenye utengenezaji wa line ya umeme ya kilometa sita. Pia katika eneo la Rigicha mkandarasi tayari yuko katika eneo na anaendelea kurekebisha line ya umeme, lakini katika kijiji ambacho amekitaja, jina lake naomba liingie kwenye Hansard kama alivyolitaja, kuna visima, vituo 30 vya kuchotea maji tayari vimekamilika na asubuhi hii DM alikuwa katika eneo hilo na amenipatia mrejesho wa kazi ambayo imeshafanyika.
Kwa hiyo, namtoa hofu Mheshimiwa Mbunge kazi inaendelea na tutahakikisha kwamba maji yanapatikana kwa usahihi zaidi, ahsante sana.
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji uliopo Mpasa, King’ombe, Kata ya Kala, Wilayani Nkasi?
Supplementary Question 6
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pale Bunda tuna mradi wa maji kutoka Nyabihu umekamilika, lakini kuna changamoto ya miundombinu na ninyi Serikali moja ya changamoto ambayo mnakabiliana nayo ni upotevu wa maji. Kuna bomba kubwa kutoka Butakale, Kata ya Bunda Stoo, unaenda Kasakwa kule kwenye tenki, Mlima Balili, inahitajika shilingi bilioni 1.7 kujenga lile bomba ambalo ni chakavu kuokoa maji yasipotee ili wananchi wa Bunda Mjini wapate maji safi na salama. Lini sasa mtatoa hizo shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya ujenzi wa bomba kuu?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Bulaya kama Serikali tukushukuru kwa kutupatia taarifa kama hiyo. Ni mkakati wa Serikali kuendelea kuboresha miundombinu chakavu yote ambayo inatusababishia kuwa na upotevu wa maji kwa sababu tunayazalisha kwa gharama na yanapokuwa yanapotea maana yake ni kwamba Serikali inaingia kwenye hasara kubwa.
Kwa hiyo, nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge nalipokea hilo na nitaenda kulifuatilia ili tuone tunafanya nini kuhakikisha kwamba bomba hilo linaenda kujengwa, ahsante sana.
Name
Cosato David Chumi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Primary Question
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji uliopo Mpasa, King’ombe, Kata ya Kala, Wilayani Nkasi?
Supplementary Question 7
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga. Wananchi wa Itimbo wanauliza, mkandarasi ameshapatikana, ni lini anaenda kuanza kazi katika Kijiji cha Itimbo?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa swali zuri. Mheshimiwa Mbunge kwa kweli tunaendelea kushirikiana vizuri na mkandarasi na ataingia site baada ya mwaka wa fedha kuanza, ahsante sana.
Name
Yahya Ally Mhata
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Primary Question
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji uliopo Mpasa, King’ombe, Kata ya Kala, Wilayani Nkasi?
Supplementary Question 8
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nanyumbu kwenye Kata ya Maratane mwaka jana, mwezi Julai tuliingia mkataba na mkandarasi wa kusambaza maji katika kata hiyo. Hadi sasa hivi mkandarasi hajaanza kazi, sababu kubwa hajapata down payment.
MWENYEKITI: Swali.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, ni lini atapata advance ili aanze kazi?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongee kidogo kwenye suala hili.
MWENYEKITI: Kwa kifupi kwa sababu majibu unaweza kuwa umeyasema.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na changamoto na wakandarasi, ni kweli kabisa kuna wengine hawajapata advance payment, lakini wengine hata kufanya ile mobilization hawajafanya, kwa hiyo, inatutia wasiwasi kuanza kuwalipa wakati hata mobilization ambayo iko kwa mujibu wa sheria kwamba tayari ukishapata mkataba unatakiwa kuanza kufanya mobilization. Kazi ambayo tunaifanya sasa hivi ni kuwasisitiza wakandarasi wote ambao tumeingia nao mikataba kuanza kufanya mobilization, tuone commitment yao na Serikali itatoa fedha kwa ajili ya advance payment kuhakikisha kwamba miradi inaanza kutekelezwa, ahsante.
Name
Michael Constantino Mwakamo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibaha Vijijini
Primary Question
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji uliopo Mpasa, King’ombe, Kata ya Kala, Wilayani Nkasi?
Supplementary Question 9
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Boko, pale Mnemela, Jimboni Kibaha Vijijini kuna tatizo la maji la muda mrefu na wananchi wamechoka kuona mabomba ambayo watu wa DAWASA wanashindwa kuyafanyia kazi. Je, Waziri unatoa agizo gani kwa Meneja wa DAWASA ili aweze kukamilisha mradi ule na watu wa Boko wapate maji?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa changamoto hii naomba nitumie fursa hii na Bunge lako Tukufu kumwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa DAWASA kwenda kulifanyia kazi eneo hili na kuweza kufanya tathmini, kujiridhisha ukubwa wa tatizo ili Serikali iweze kuchukua hatua na wananchi waendelee kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana.