Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. John Danielson Pallangyo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Mashariki
Primary Question
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:- Je, lini Serikali itatenga fedha kumalizia usambazaji wa maji safi na salama Kata ya King’ori, Wilayani Meru hususani katika Vijiji vya Meru kwa Philipo?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali na nitumie nafasi hii kuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu mpendwa kwa juhudi kubwa ambayo tunaiona jimboni ya kutaka kumaliza kabisa tatizo la maji. Tunavyozungumza sasa hivi mtambo wa kuchimba maji visima virefu kwa ajili ya kufuata maji ya ardhini huko jimboni na kazi inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna shida kubwa sana ya maji katika Tarafa ya King’ori ambayo imebeba Kata za Kikatiti, Majengo, Malula, King’ori, Maruvango, Leguruki, Ngarenanyuki, Uwiro na Ngabobo. Pia eneo hilo maji yana- fluoride...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, swali.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza changamoto hizi za maji eneo hilo? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. John Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafurahi kuona Mheshimiwa Mbunge anatambua kazi kubwa ambayo inafanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kweli mtambo upo na kama ambavyo nilijibu katika majibu mengine, mitambo hii sasa wataalamu tayari wameshapatikana wanaingia site kuhakikisha kwamba visima vinaanza kuchimbwa. Pamoja na hilo, Skimu ya Makilenga inahudumia takribani 50% ya Tarafa ya King’ori. Kwa hiyo, tumwombe Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana kuhakikisha kwamba changamoto hii inaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sasa pia Serikali inashirikiana na mdau wa maendeleo kutoka Korea kuhakikisha kwamba kuna madini ya fluoride katika eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge ameongelea na madini hayo sasa tunaenda kufanya mchakato wa kuyaondoa na kuchuja na kuhakikisha kwamba wananchi wa eneo lile wanapata maji ambayo hayatokuja kuwa na madhara katika afya zao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, Serikali tayari imeshaanza kufanya kazi hiyo, nakushukuru sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved