Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Primary Question

MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:- Je, lini Halmashauri ya Wilaya ya Uyui itagawanywa na kutoa Halmashauri mpya ya Kizengi?

Supplementary Question 1

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, Mheshimiwa Rais alipokuja Mkoa wa Tabora tulimpelekea ombi maalumu la kuanzisha Halmashauri mpya ya Kizengi na akatoa maelekezo kwa mkoa na wilaya kuandika maombi hayo na kuyapeleka Wizarani na mkoa ulishafanya hivyo na maombi yale yameshawasilishwa kwa Katibu Mkuu, TAMISEMI. Nataka Waziri aniambie, je, hiyo barua imefika kwao au bado?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya Uyui, hasa Jimbo la Igalula katika Kata za Loya, Tula Miswati, Mbale wanapata adha sana ya kupata huduma katika Halmashauri yetu kutoka kilometa nyingi wanatembea kufuata huduma. Hamuoni haja kama Wizara kumshauri Mheshimiwa Rais ili aweze kuitangaza Halmashauri ya Kizengi ili kuongeza huduma kwa wananchi?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepokea kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora maombi hayo aliyoyazungumza Mheshimiwa Mbunge na inaendelea kuyafanyia uchambuzi kulingana na vigezo vilivyopo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barua hiyo ilishafika Serikalini Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kipaumbele cha Serikali kwa wakati huu kwa mujibu wa Ibara ya 9(a) (4) ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi wa Mwaka 2020 ni kuimarisha Serikali za Mitaa ili ziweze kutimiza wajibu wao. Kwa mantiki hiyo Serikali kwa wakati huu imejikita katika kuimarisha maeneo ya utawala yaliyopo kwa maana ya kuajiri watumishi katika maeneo ambayo yenye upungufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, Serikali itatengeneza au kuweka miundombinu muhimu kama majengo ya ofisi, kupeleka shule, huduma za afya, maji, barabara na umeme. Kwa hiyo, kwa wakati huu Serikali imejielekeza katika kuboresha mamlaka zilizopo tofauti na kuanzisha mamlaka mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kuendelea kuimarisha miundombinu ya huduma za kijamii na kiuchumi katika maeneo waliyonayo ili huduma ziweze kuwafikia wananchi wote karibu na maeneo yao ili kuongeza ufanisi na huduma bora zaidi kwa wananchi.