Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Omar Issa Kombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wingwi

Primary Question

MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: - Je, lini Serikali itafanyia kazi changamoto ya kodi na tozo kwenye fedha za Mfuko wa Jimbo kwa upande wa Zanzibar?

Supplementary Question 1

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri ambayo kwa kweli yamekuwa ni majibu ya kufanana siku zote na wala hayaleti matumaini kwa Wabunge wote kutoka Zanzibar, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali mmekiri kwamba changamoto ni sheria na sisi ndio watunga sheria: Ni lini mtaleta Muswada hapa Bungeni ili kubadilisha sheria hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba Mfuko huu unakatwa tozo kwa sheria mbili; Sheria ya Zanzibar na Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania: Je, hamuoni haja ya kukaa pamoja ili kuangalia ni namna gani ya kutatua changamoto hii ili iweze kukatwa tozo kwa upande mmoja tu? Ahsante. (Makofi)

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar Issa Kombo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimwambie tu kwamba awe na matumaini kwa sababu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, inafuata kabisa misingi ya Mwanafalsafa Bentham, mtaalamu wa sheria aliyesema, “Laws should provide minimum pain and provide maximum pleasure.” Kwa msingi huo ni kwamba, sheria hizi zilizotungwa siyo Msahafu wala Biblia Takatifu. Zinaweza kubadilishwa kulingana na mahitaji yaliyopo, lakini pia kutatua changamoto ambazo zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa lugha ya Kilatini wanasema, “Ubi societas, ibi jus, ibi ius ubi societas” kwa maana ya kwamba sheria ni zao la jamii na jamii ndiyo inayozaa sheria. Sasa Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ameleta hoja hii ndani ya Bunge na utakumbuka vizuri katika Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mheshimiwa Waziri alijibu hapa na akaeleza kwamba suala hilo walilitolea ufafanuzi. Pia, akasema Serikali iko tayari kukaa na wataalamu kwa upande wa Zanzibar, kukaa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar; ZRA, TRA na Ofisi yetu ya Wizara ya Fedha ili kuweza kuangalia ni sehemu gani wanaweza wakarekebisha na kuhakikisha kwamba pande hizi zote wanapata nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mwisho wa siku fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ni kwa ajili ya maendeleo ya mwananchi. Pia kodi inayokatwa ni kwa ajili ya maendeleo ya mwananchi na nchi kwa ujumla. Kwa hiyo, hivi vyote kwa pamoja tutaweza kuviangalia. Nimtoe wasiwasi kwamba Serikali iko makini na tutalishughulikia ili kuweza kuhakikisha tuna-provide maximum pleasure na tunaondoa hizo minimum pain, ahsante.