Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka walimu wa kutosha katika shule mpya kumi za msingi na sekondari zilizojengwa Vwawa?
Supplementary Question 1
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi, hesabu na biashara ambayo ni 172 katika shule za sekondari mpya; na kwa kuwa katika shule za msingi kuna upungufu wa walimu 693.
Je, zipi hatua za Serikali za muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu wa kukabiliana na changamoto hii ya upungufu wa walimu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa katika maeneo mengi kuna walimu wengi ambao wamehitimu na bado hawana ajira, upi mkakati wa Serikali wa kuwatumia hao walimu kwa muda mfupi ili waweze kusaidia katika kupunguza changamoto ya upungufu wa walimu? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ni kweli katika shule zetu kote nchini zikiwemo shule hizi za Jimbo la Vwawa kuna upungufu wa walimu wa sayansi, hisabati lakini na masomo mengine kama masomo ya biashara, lakini Waheshimiwa Wabunge ni mashuhuda kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeajiri walimu kwa wingi kwa makumi elfu katika kipindi cha miaka hii mitatu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo walimu wameendelea kuajiriwa na kupelekwa katika shule hizo Serikali itaendelea kuajiri kadri kibali cha ajira kinavyojitokeza na kipaumbele cha ajira hizi huwa ni walimu wa sayansi, walimu wa hisabati na masomo mengine yenye upungufu mkubwa zaidi. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge zoezi hilo linaendelea na tutahakikisha kwamba walimu wanafika kupunguza upungufu wa walimu katika shule hizo.
Mheshimiwa Spika, lakini pili, Serikali ilishatoa mwongozo wa namna ambavyo halmashauri zinaweza kutumia mapato ya ndani kuingia mikataba na walimu ambao wamehitimu wako katika maeneo yao kwa ajili ya kufundisha. Sisi sote tumeshuhudia kote nchini shule nyingi zina walimu ambao wameajiriwa kwa mikataba na wanaendelea kufundisha wakisubiri ajira za kudumu. Nitumie nafasi hii kusisitiza na kuhamasisha Wakurugenzi wahakikishe wanatumia fursa hii vizuri, ahsante
Name
Deodatus Philip Mwanyika
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Njombe Mjini
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka walimu wa kutosha katika shule mpya kumi za msingi na sekondari zilizojengwa Vwawa?
Supplementary Question 2
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nashukuru; Halmashauri ya Mji Njombe ambayo ina vijiji na miji, mwaka jana haikupata mgao kama halmashauri nyingine za miji ambazo zina vijiji; je, Serikali ina mpango gani kwenye mgao wa safari kuzifikiria tofauti ili zipate walimu wa kutosha?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, wakati wa kupeleka walimu katika vituo vyetu baada ya ajira kuna vigezo ambavyo vinazingatiwa lakini kigezo muhimu ni upungufu mkubwa zaidi wa walimu katika halmashauri hizo na katika shule hizo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mara ajira zitakapojitokeza tutahakikisha tunazingatia vigezo na yale maeneo ambayo yana upungufu mkubwa katika halmashauri ya Mji wa Njombe yatapelekewa walimu ili kupunguza gap hiyo ya walimu katika shule hizo.
Name
Issaay Zacharia Paulo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka walimu wa kutosha katika shule mpya kumi za msingi na sekondari zilizojengwa Vwawa?
Supplementary Question 3
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, hivi sasa kuna upungufu mkubwa sana wa nyumba za walimu; je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga maboma yote ya nyumba za walimu katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu na kwingineko nchini?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba kuna upungufu mkubwa wa nyumba za walimu na tayari imeshaanza mkakati na utekelezaji unaendelea wa kujenga nyumba za three in one, two in one katika shule zetu lakini pia maboma ya nyumba za walimu katika shule zetu yameshaanza kutambuliwa yote na kuna mpango kabambe wa kuhakikisha shule zinakuwa na nyumba za walimu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi hilo litafanyika na walimu wetu watapata nyumba katika shule hizo, ahsante.
Name
Neema Kichiki Lugangira
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka walimu wa kutosha katika shule mpya kumi za msingi na sekondari zilizojengwa Vwawa?
Supplementary Question 4
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Bukoba Mjini inahitaji walimu wa sayansi 386 lakini hivi sasa kuna walimu 146, hivyo tuna upungufu wa walimu wa sayansi 240.
Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba Bukoba Mjini tunapata walimu wa sayansi wa kutosha? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Bukoba Mjini ni moja ya halmashauri ambazo katika ajira zote za walimu zilizopita pia walipata walimu wa masomo ya sayansi, lakini ni kweli kwamba walimu wale bado hawatoshelezi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kila ajira zitakapojitokeza tutahakikisha tunaipa kipaumbele Halmashauri ya Bukoba Mjini ili walimu wa sayansi waweze kupatikana na kuboresha ikama katika shule zetu zote, ahsante.