Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Primary Question

MHE. STANSLAUS S. MABULA K.n.y. MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA aliuliza:- Je, lini mgogoro kati ya wananchi wa Kiwanja cha Ndege Mwanza na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege - Mwanza utatatuliwa?

Supplementary Question 1

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali ilishakuwa na makubaliano ya awali kuchukua eneo ambalo siyo zaidi ya ndani ya meta 700 kulipa fidia na sasa inaonekana itakwenda zaidi ya kata tano zikiwemo Kata za Shibula pamoja na Bulyanhulu na wakazi zaidi ya 1,400, je, Serikali haioni kuchukua eneo lote hili kwa wakati mmoja kutaathiri maisha ya baadhi ya wananchi ambao wako nje kabisa ya eneo la uwanja wa ndege?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali kwa kuanza ujenzi wa jengo la abiria, ni lini mkakati wa Serikali kuhakikisha Uwanja wa Ndege wa Mwanza na wenyewe unakuwa moja ya viwanja vya Kimataifa hapa nchini? Nashukuru.

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la pili kisha nirudi swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inatambua umuhimu wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza kuufanya wa Kimataifa na tayari mambo kadhaa yameanza kufanyika. La kwanza, tuko kwenye hatua za ndani za documentation. Ili uwanja uweze kuwa wa Kimataifa, kuna taratibu za kisheria ambazo lazima zizingatiwe.

Mheshimiwa Spika, la pili, ni pamoja na kuondoa wavamizi wapatao 1,000 katika uwanja huu ili waweze kupisha kiwanja hicho kiweze kuwa salama. Pale kuna milima na maeneo mbalimbali ambayo wananchi wamevamia. Kwa hiyo, huwezi kukifanya cha kimataifa wakati huo huo usalama wa kiwanja uko mashakani.

Mheshimiwa Spika, la tatu, tunafanya kazi ya uboreshaji wa miundombinu. Kama unavyofahamu, tarehe 28 mwezi huu Waziri wetu Mheshimiwa Mbarawa alikwenda kushuhudia ujenzi wa jengo la abiria. Iko mikakati mingi, lakini nimetaja mitatu ya kuufanya uwanja huu kuwa wa kimataifa.

Mheshimiwa Spika, sasa nikirudi kwenye swali lake la kwanza, nafikiri litakuwa limeshajibiwa na hoja hii ya pili, kwa sababu hatuwezi kuacha eneo ambalo nimeshalisema pale juu, kwa sababu tu tunataka tuufanye uwanja wa kiamataifa. Kwa hiyo, lazima watu wapishe ili tuweze kuupa hadhi inayostahili, ahsante.