Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Martha Jachi Umbulla
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:- Kamati za Fedha za Mipango za Halmashauri za Wilaya ni Kamati muhimu sana kwa Wabunge wote kushiriki bila kujali ni wa Viti Maalum au wa Jimbo kwa sababu zinashughulika na masuala ya fedha, bajeti na mipango ya miradi ya maendeleo; na kwa muda mrefu sasa Wabunge wa Viti Maalum wamekuwa wakiomba kuondolewa kwa sheria kandamizi na ya kibaguzi ya kuwazuia kushiriki katika Kamati hizo:- (a) Je, Serikali iko tayari kusikiliza kilio cha Wabunge wa Viti Maalum ili kuwaruhusu kushiriki kwenye Kamati hizo? (b) Je, Serikali iko tayari kufuta sheria hiyo kandamizi na yenye ubaguzi ambayo haina tija na hasa ikizingatiwa kuwa ilitungwa mwaka 1998 wakati ambao Ubunge wa Viti Maalum bado haujaanza?
Supplementary Question 1
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zote za Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wananchi vijijini zinapita kwenye Halmashauri za Wilaya na katika vikao vya Halmashauri za Wilaya hasa Kamati hiyo ya Fedha na Mipango Wabunge wa Viti Maalum hawashiriki na ndiyo watu wenye dhamana na maendeleo ya wanawake.
Kwa kuwa sheria hiyo iliyotungwa ambayo inawakataza Wabunge wa Viti Maalum kuingia kwenye Kamati hizo ilitungwa zamani sana kabla hata utaratibu wa Ubunge wa Viti Maalum haujaanza bali kulikuwa na Wabunge wa Majimbo na Wabunge wa Kuteuliwa na Rais; na kwa kuwa mwaka jana kwenye Bunge la Kumi, Mheshimiwa Mwanri aliyekuwa Naibu Waziri alipokuwa anajibu swali hapa Bungeni, alitueleza kwamba sheria hiyo ni kandamizi na tunahitaji kuileta hapa Bungeni ili tuirekebishe Wabunge wa Viti Maalum washiriki.
Je, Serikali italeta lini hiyo sheria ili Wabunge wa Viti Maalum waweze kushiriki katika Kamati hii muhimu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Halmashauri zetu za Wilaya hasa kwa Mkoa wetu wa Manyara zinatenga asilimia kumi za fedha kwa ajili ya miradi ya wanawake. Utaratibu na mfumo wa utoaji wa fedha hizo kwa ajili ya miradi ya wanawake hauko vizuri na kuna upotevu mkubwa sana wa fedha hizo za Serikali.
Je, ni kwa nini Madiwani wa Viti Maalum wakisaidiana na Wabunge wao wasisimamie kikamilifu utoaji na urejeshaji wa fedha hizo ili ziweze kuwafikia walengwa?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martha kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali kila kitu kipo kwa mujibu wa sheria na kanuni zake. Katika jibu langu la msingi katika eneo la pili nikasema mchakato unaweza ukaendeshwa kwa kuwashirikisha wadau. Hili la kuwashirikisha wadau kama nilivyosema lina umuhimu mkubwa sana. Katika maeneo mengine kwa mfano nikichukua Jimbo langu mimi la Kisarawe, Mbunge wangu wa Viti Maalum anaingia katika Kamati ya Fedha na sehemu zingine wanaingia katika Kamati hii, ina maana hivi sasa katika zile nafasi mbili Mwenyekiti anaweza akateua Mbunge wa Viti Maalum kuweza kuingia pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kusimamia fedha ni wajibu wa Madiwani na Wabunge wahusika katika eneo hilo. Kwa upana wa jambo hili, ndiyo maana nimesema wadau lazima washirikishwe. Kuna baadhi ya Majimbo, mfano Jimbo la Ilala, lina Wabunge wa Majimbo watatu, lina Madiwani wa Viti Maalum wasiopungua watano, kwa hiyo ukiangalia hapo, ndiyo maana nasema lazima wadau washirikishwe kuona jambo hilo linakaajekaaje na kuangalia ni jinsi gani tutafanya Kamati ya Fedha iweze kufanya vizuri. Kwa mfano, kwa hali ya sasa hivi ukisema Jimbo la Ilala Wabunge wote wa Viti Maalum waingie katika Kamati ya Fedha mtapata sura hapo, ndiyo maana nasema lazima sheria hiyo tuitazame kwa upana na wadau washiriki kila mmoja katika eneo lake kuangalia jinsi gani tutafanya, hilo ni jambo la msingi lakini kwa sasa hivi sheria inasimama hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu asilimia tano ya akina mama na siyo ya akina mama peke yake, ni ya vijana na akina mama. Jambo hili nililisema katika vikao mbalimbali kwamba jukumu la Kamati ya Fedha ni kuhakikisha kwamba fedha zinazokusanywa kutoka own source ziweze kuyafikia yale makundi ya akina mama na vijana. Kwa bahati mbaya hata katika kaguzi mbalimbali zilizopita hili ni miongoni mwa eneo lenye changamoto kubwa na ndiyo maana tumetoa maelekezo kuhusu suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasema agenda ya kuhakikisha akina mama na vijana wanapata fedha hii ni yetu sote. Ndiyo maana bajeti ya mwaka huu criteria tuliyotumia kuhakikisha Halmashauri zote zinatengewa bajeti ni kuhakikisha kwamba wanatenga asilimia tano ya vijana na akina mama na walemavu watakuwa katika mchakato huo. Kwa hiyo, hili ni agizo la jumla kwamba kwa vile bajeti tumeipitisha basi kila Halmashauri ihakikishe inasimamia asilimia tano za akina mama na tano za vijana ziweze kuwafikia walengwa.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved