Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ritta Enespher Kabati
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:- Je, lini Barabara ya Mtandika hadi Nyanzwa - Kilolo itajengwa kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake. Naomba Barabara hii iweze kupitika kwa sababu hali yake ni mbaya sana. Sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Barabara ya Ilula – Image - Ibumu ni ahadi ya Serikali ya muda mrefu sana, lakini kwa sasa hivi hali yake ni mbaya sana, haipitiki na wananchi wamekuwa wakipata shida sana. Je, lini Serikali itatimiza ahadi yake? Kwa sababu hii barabara ikijengwa ni pamoja na kumuenzi Eng. Patrick Mfugale ambaye anaishi katika hilo eneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; Barabara ya Kitowo – Kihesa - Mgagao – Mwatasi - Masisiwe ambayo inakwenda mpaka Idete ni barabara ya kiuchumi, lakini ina hali mbaya sana na haipitiki. Je, Serikali iko tayari angalau kujenga zile sehemu korofi tu ili iweze kupitika wakati huu kwa sababu mabasi hayapiti? Wananchi wanapata shida sana hata wanaokwenda kujifungua, wagonjwa na wazee. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuja katika Mkoa wetu wa Iringa ajionee hali mbaya ya barabara jinsi ili aweze kusaidia wananchi, nao waweze kufaidika na Serikali yao na uchumi uweze kujengeka?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anafanya kazi kubwa sana ya kuwatetea wananchi wake. Mara kwa mara tumekuwa tukiwasiliana akinieleza changamoto za miundombinu katika eneo lake la uwakilishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali lake la kwanza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Ilula – Image – Ibumu tayari imeanza kujengwa baada ya kupokea fedha jumla ya shilingi milioni 150 za dharura. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha hizi tayari zimeshatolewa na ujenzi wa barabara hii umeshaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Barabara hii ya Kitowo – Masisiwe – Mwatasi imetengewa bajeti ya shilingi milioni 36.8 katika Mwaka wa Bajeti 2023/2024 kwa ajili ya kuchonga kilomita nane za barabara na kuweka kifusi kwa kilomita mbili kwenye maeneo korofi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hizi kwa Uchumi, lakini pia kwa ustawi wa wananchi na inafanyia kazi kwa kadri fedha inavyopatikana kwa kufanya marekebisho na kujenga katika maeneo ya barabara ambazo zina changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, nikitoka hapa nikikaa kwenye kiti changu tutazungumza ili tupange ratiba nzuri ya mimi kufika katika eneo lake ili kuona changamoto za wananchi na kuzitafutia suluhu. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved