Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mwanne Ismail Mchemba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Primary Question

MHE. MWANNE I. MCHEMBA (K.n.y. MHE. HALIMA ALI MOHAMMED) aliuliza:- Serikali imejipanga kupiga vita suala la ajira kwa watoto na imekuwa ikiunga mkono matamko ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na ajira za watoto. Je, kupitia Mradi wa TASAF III Serikali ina mikakati gani ya makusudi kuwasaidia watoto na tatizo la ajira za utotoni kwa upande wa Zanzibar?

Supplementary Question 1

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Kwa kuwa ongezeko la ajira kwa watoto wadogo ni kubwa sana hapa nchini; na kwa kuwa tatizo hilo kuchangiwa na kuvunjika kwa ndoa kwa kutokuwa na msingi na kuachiwa akina mama kulea hao watoto. Je, Serikali ina mpango gani wa makusudi na wa haraka kuleta mabadiliko ya sheria ya mwaka 1971 ili wanawake na watoto hawa waweze kupata haki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwa kuwa TASAF III imeonesha mpango mzuri sana na mimi nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa sababu kwenye mashamba makubwa watoto hao wapo wengi na wanaonekana kama vile kwenye mashamba ya tumbaku, kahawa, chai, pamba na kadhalika, je, Waziri yuko tayari kuwakusanya hawa watoto na kuwapa elimu ya kutosha?

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa swali lake la kwanza kuhusiana na kufanya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, bahati nzuri suala hili limekuwa likizungumzwa katika nyakati mbalimbali na hata katika Bunge hili na Mkutano huu wa Tatu, Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria amelisemea sana, lakini vilevile Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto pia ameweza kulizungumzia.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kurudia kwa mara nyingine tena, ni kweli sheria hii ilionekana kuna upungufu. Ukiangalia viko baadhi ya vifungu vinavyoruhusu masuala mazima ya ndoa za utotoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa kutambua kwamba katika masuala haya ya ndoa kuna mkanganyiko wa masuala ya kimila na kidini, ikaonekana kwamba ni vema suala hili likapatiwa suluhu kwa kupata maoni ya wananchi wengi zaidi kupitia mchakato wa White Paper. Mwanzo wakati zoezi hili Wizara ya Katiba na Sheria ilipotaka kulianza, taratibu zote karibia zilikuwa zimeshakamilika, lakini ikawa imeingiliana na mchakato wa Mabadiliko ya Katiba. Ikaonekana itakuwa si wakati mzuri kuwachanganya wananchi, huku wanatakiwa watoe maoni kuhusiana na Katiba Mpya lakini wakati huo huo unawapelekea zoezi lingine kuhusiana na marekebisho ya Sheria ya Ndoa. Vilevile ilionekana kwamba huenda wakati ule kwenye kukusanya maoni ya Mabadiliko ya Katiba wananchi wangeweza kulisemea jambo hili lakini kwa kiasi kikubwa halikusemewa sana. Kwa hiyo, niseme tu kwamba kwa upande wa Wizara ya Katiba na Sheria bado wanasubiria wakati mzuri zaidi wa kuweza kulipeleka lakini ni lazima liende kupitia Waraka wa Maoni kupitia White Paper.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili kwamba je, Serikali iko tayari kutoa elimu kwa watoto ambao wamekuwa wakifanya ajira mbalimbali za utotoni, niseme tu kwamba kupitia Wizara ya Kazi kwa Mheshimiwa Jenista, wamekuwa wakifanya kazi hii na wanaendelea kufanya kazi hii kuhakikisha kwamba watoto hawa ambao wako katika ajira za utotoni wanaelimishwa, lakini zaidi kuhakikisha kwamba wazazi wao wanapewa elimu hii. Ndiyo maana kupitia TASAF kama nilivyoeleza, nichukulie tu kwa upande wa Zanzibar, zaidi ya watoto laki moja na mbili wamekuwa wakinufaika na ruzuku hii ili kuwawezesha kwenda shule.
Kwa hiyo, ni imani yangu bado kupitia Serikali kwa ujumla wake na mipango mbalimbali na TASAF ikiwemo tutahakikisha tunatoa elimu hii, lakini vilevile kuona ni kwa namna gani watoto wengi zaidi wanaweza kunufaika nayo. Nakushukuru.

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWANNE I. MCHEMBA (K.n.y. MHE. HALIMA ALI MOHAMMED) aliuliza:- Serikali imejipanga kupiga vita suala la ajira kwa watoto na imekuwa ikiunga mkono matamko ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na ajira za watoto. Je, kupitia Mradi wa TASAF III Serikali ina mikakati gani ya makusudi kuwasaidia watoto na tatizo la ajira za utotoni kwa upande wa Zanzibar?

Supplementary Question 2

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa TASAF III imekuwa ikihamasisha sana hizi kaya maskini kujiunga na Mfuko wa Bima za Jamii (CHF). Je, mpaka sasa ni kaya ngapi zimeweza kujiunga na huu Mfuko huu?

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa tu niombe uniruhusu niweze kutoa maelezo ya utangulizi kidogo kabla sijajibu hoja yake. Kumekuwa na hoja na watu wengi wamekuwa wakitoa ushauri kwamba katika hizi kaya ambazo zinanufaika na ruzuku hii ya uhawilishaji, walazimishwe kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii.
Kwanza kabisa niseme duniani kote katika taratibu za uendeshaji wa mipango ya uhawilishaji wa fedha katika jamii huwa ni hiari. Kwa hiyo, tunachokifanya sisi kama TASAF ni kuhakikisha kwamba katika kila siku wanapoenda kupokea malipo tunawaelimisha kuhusiana na umuhimu wa kuweza kujiunga na Mfuko huu wa Bima ya Afya. Hadi sasa kaya 54,924 kutoka katika Halmashauri 28 zimeweza kujiunga na Mfuko huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu pongezi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chato ambayo zaidi ya 90% ya walengwa wake wameshajiunga na Mfuko wa Bima ya Afya. Nitoe pia pongezi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale ambapo 60% ya walengwa wake tayari wameshajiunga na Mfuko wa Bima ya Afya.
Vilevile nitoe pongezi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi, Halmashauri au Manispaa ya Mtwara pamoja na Kibaha lakini na nyingine nyingi. Niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge na ninyi pia mtusaidie kuendelea na uhamasishaji ili kuhakikisha kwamba walengwa hawa wanaweza kujiunga ili waweze kupata huduma ya matibabu ya afya pale wanapohitaji. Nakushukuru.