Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Primary Question

MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: - Je, lini zoezi la kuhamia Dodoma litakamilika na Taasisi ngapi zimeshahamia Dodoma?

Supplementary Question 1

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini vile vile nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia vyema zoezi hili la Serikali kuhamia Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, pamoja na kwamba taasisi 65 zimeshahamia hapa Dodoma, lakini mwisho kabisa wa taasisi zote kuhamia Dodoma ni lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Makao Makuu ya Nchi ambako viongozi wengi wa Serikali wanafanya kazi ni lazima kuwe na makazi yao rasmi. Je, ujenzi wa makazi rasmi ya viongozi wa Serikali utaanza lini?

Name

Ummy Hamisi Nderiananga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Naibu Spika, napokea pongezi hizo za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu lini mwisho wa taasisi za Serikali kuhamia Dodoma, kama nilivyojibu katika swali la msingi la Mheshimiwa Kenneth Nollo kwamba tunaendelea na uchambuzi. Taarifa itakapokamilika, tutawaambia ni taasisi ngapi zimeshahamia na ngapi zimebaki. Tunatarajia mwaka 2025 taasisi zote ziwe zimeshahamia Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali lake la pili, kwanza naendelea kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri. Nimhakikishie kwamba Serikali ilianza ujenzi wa nyumba za viongozi kuanzia mwaka 2021/2022. Kupitia Wakala wa Majengo (TBA) tulijenga nyumba 20 na Septemba, 2023 nyumba 150 za watumishi zilizinduliwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tuko kwenye zoezi la kupanga eneo ambalo tumelitwaa kwa ajili ya kujenga nyumba za viongozi wa Serikali na watumishi. Sasa hivi tuko kwenye hatua ya kujipanga kwa kupitia hao wenzetu wa TBA watuainishie vizuri, na tutakuwa na ekari 4,654. Tumetwaa eneo kati ya Mji wa Serikali Mtumba na Ikulu hapo kwa ajili ya kujenga nyumba hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Watanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tunaendelea vizuri na uendelezaji wa Mji wa Serikali Mtumba na kila jambo linaendelea vizuri. Kwa hiyo, niwatoe mashaka na niwakaribishe sekta binafsi, ahsante.