Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Najma Murtaza Giga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: - Je, kwa nini Tamaduni za kigeni zimetawala sanaa zetu kuliko utamaduni wetu wakati BASATA ipo kuhimiza na kukuza utamaduni wetu?

Supplementary Question 1

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; pamoja na jitihada nzuri zinazofanywa na Serikali katika kulinda tamaduni za Kitanzania nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kwamba kuna baadhi ya filamu watoto wa kiume wana-act au wanaigiza kama watoto wa kike: Je, BASATA na Serikali hawaoni kwamba hili linaweza kuchochea watoto wetu wa kiume waone kwamba kuwa watoto wa kike ni jambo la kawaida? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kuhusu maudhui na miziki au filamu na mziki zilizomo ndani ya mabasi yaendayo mikoani. Mavazi yanayovaliwa na vijana wetu mle ndani hasa watoto wa kike ni nusu ya utupu. Je, Serikali au BASATA haioni kwamba hii ni kinyume cha sheria na kwamba ni tabia mbaya ambayo inaporomosha maadili ya nchi yetu? (Makofi)

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwenye swali la kwanza lina mtego kidogo kwa sababu kazi ya wasanii pamoja na mambo mengine ni kuburudisha. Sasa wasanii wanaweza wakavaa uhusika wa aina yoyote. Wasanii mara nyingi wameimba nyimbo wakiigiza kuwa madaktari, wakiigiza kuwa waganga wa kienyeji, wakiigiza kuwa walevi, walioathirika na kadhalika. Kwa hiyo, kuvaa uhusika ni jambo moja ambalo limekaa kimtego na namna ya Serikali kulishughulikia ni kuangalia tu namna ambavyo kama litakuwa limezidi na linaakisi kupelekea kwenye kuisukuma jamii kufanya vitendo visivyofaa hapo ni lazima tutachukua hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunaendelea kufuatilia kwa karibu kupitia Baraza la Sanaa la Taifa kuhakikisha kwamba maudhui yaliyopo katika filamu na nyimbo zetu hayakiuki misingi ya maadili ya Mtanzania na tunachukua hatua kila wakati inapofaa kufanya hivyo. Hata hivyo, tunaendelea kuwaelimisha wasanii kwa namna moja ama nyingine kuhusiana na jambo hili na kuhakikisha kama na wao wanabaki kwenye misingi na Maadili ya Kitanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, jibu hili pia linakwenda kwenye swali lake la pili kuhusiana na mavazi ambayo yanakuwa ni nusu uchi kwenye nyimbo zilizorekodiwa ama filamu ambazo zinaoneshwa kwenye mabasi. Tunachoendelea kukifanya ni kuhakikisha maudhui yote yaliyoko katika nyimbo ikiwemo video zake na filamu za Kitanzania hayakiuki maadili ya Kitanzania ili kuepusha tatizo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelisema, nakushukuru. (Makofi)

Name

Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Primary Question

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: - Je, kwa nini Tamaduni za kigeni zimetawala sanaa zetu kuliko utamaduni wetu wakati BASATA ipo kuhimiza na kukuza utamaduni wetu?

Supplementary Question 2

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Je, ni upi mkakati wa Serikali kuanzisha kampeni maalum kuondoa kasumba ambayo imejengeka kwetu sisi Watanzania kwamba tunapotumia mambo ya kimagharibi sana ni tafsiri ya kuonesha kwamba tumestaarabika? Kwa mfano, mtu unapoonekana unaweza kuongea Kiswahili peke yake na huwezi kuongea Kiingereza wewe hujasoma, wakati Wachina na Wafaransa hawajui Kiingereza na bado wanaheshimika; au kuonekana ukiwa unatumia mvinyo ambao unatoka nchi za magharibi wewe umestaarabika na ni msomi, lakini ukitumia mivinyo yetu ya ndani ya nchi wewe ni mshamba…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sichalwe uliza swali lako. Mheshimiwa Waziri.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nimemwelewa vizuri ni kuhusu umagharibi kuingia kwenye tamaduni zetu na maisha yetu ya kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, dunia imekuwa kama Kijiji, kwa hivyo ni suala la ridhaa ya mtu na namna ambavyo anataka kuendesha maisha yake, lakini sisi ambacho tunakifanya ni kuhakikisha tunaendelea kuelimisha. Pamoja na mambo mengine kwa sasa tunafanya filamu ambazo zina maudhui ambayo yanaonesha umuhimu wa kuweka mbele utamaduni wetu kuliko kuiga tamaduni za kimagharibi. Tunaendelea na suala hili kupitia Baraza la Sanaa la Taifa, Baraza la Kiswahili la Taifa na Bodi ya Filamu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, hili jambo sisi tunaendelea kulifanya japo ni ridhaa ya mtu mwenyewe anaamua anavyotaka maisha yake yafanyike, lakini tutaiweka katika namna ambayo itaonesha kufuata utamaduni wa kimagharibi siyo ujanja wowote na unaweza kuendelea kufuata utamaduni wa Kitanzania na ukaonekana una class unayotaka ionekane unayo, ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Michezo.

WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini niongezee kwenye hoja kwamba ili kuhakikisha wasanii wetu wanazingatia Maadili ya Kitanzania, tumeenda kubadilisha kanuni pale BASATA, tumeingiza wadau wengine ambao wanahusika kwenye production ya hizo video na nyimbo, kwa sababu mwanzoni tulikuwa tunamwadhibu msanii wakati producer ndio anatengeneza ile content na ndio anamwambia msanii avae vipi na a-behave vipi? Sasa hata producer na wadau wengine wa kwenye production tumewaingiza katika mfumo wa kanuni na wanaadhibiwa ili kuhakikisha tunakomesha vitendo hivyo. (Makofi)

Name

Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Primary Question

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: - Je, kwa nini Tamaduni za kigeni zimetawala sanaa zetu kuliko utamaduni wetu wakati BASATA ipo kuhimiza na kukuza utamaduni wetu?

Supplementary Question 3

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tunapambana sana na maadili ya watoto, Wizara haioni sasa ni wakati wa kuzuia ule uhusika ambao unapelekea kuchochea watoto kuingia kule kwenye tabia zile mbaya hasa wale wanaume ku-act kama wanawake na baadaye kupelekea watoto kuona tabia za kishoga ni za kawaida?

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilijibu wakati najibu moja ya maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Giga, jambo ni lile lile ambalo Wizara inalitilia mkazo na inalifanya kwa nguvu nyingi, kuhakikisha tunatoa elimu kwa wasanii wetu. Halikadhalika tunachukua hatua pale inapostahili kufanya hivyo kama ambavyo tunaona kwamba wanakiuka maadili ya kitanzania. Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo tunaendelea kulifanya kwa nguvu nyingi na tunahitaji ushirikiano wa kila Mtanzania kuhakikisha tunakemea jambo hili, ahsante.