Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dorothy George Kilave

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Temeke

Primary Question

MHE. DOROTHY G. KILAVE K.n.y. MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza: - Je, lini Barabara za Tinyango, Machimbo, Kisiwani, Mapemba, Federation, Kwa Mzala na Kwa Masista, Kata ya Chamazi zitajengwa?

Supplementary Question 1

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, wakati tunasubiri mpango wa Serikali wa hizi barabara nyingine kujengwa, je, hamuoni ipo sababu ya kurudisha mawasiliano katika barabara ya Tinyango kwa sababu kuna uharibifu mkubwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya Mama Kibonge katika Kata ya Buza Jimboni Temeke?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri sana yenye lengo la kutetea wananchi, lakini kuhusiana na swali lake la kwanza naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii ya Tinyango itajengwa kwa kutumia mapato ya ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke pamoja na Meneja wa TARURA wa Temeke kuhakikisha kwamba wanatangaza kazi zote zile zilizobakia ambazo ni za matengenezo na zinatokana na fedha ya mapato ya ndani katika halmashauri wazitangaze haraka iwezekanavyo ili wakandarasi wapatikane waanze kuzijenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, barabara hii ya Tinyango ni miongoni mwa barabara moja ambayo ipo katika utaratibu huo na kwa wakati huu naomba niendelee kusisitiza kwamba wananchi waweze kutumia njia mbadala ambazo zimewekwa. Kuna njia mbili; kuna njia ile ya Mbande - Kisiwani, lakini kuna ile ya Uvikiuta – Tinyango. Kwa hiyo, mpaka ile barabara ya Tinyango itakaporudishiwa mawasiliano wananchi waweze kutumia barabara hii. Namwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke aharakishe utaratibu wa kuanza ujenzi wa barabara hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka wa bajeti kuhakikisha inafanya matengenezo na kuboresha barabara zetu hizi za wilaya. Nimhakikishie kwamba barabara yake hii ambayo ipo Buza na yenyewe ipo katika utaratibu wa kufanyiwa matengenezo katika mwaka huu wa fedha. Namwahidi itatengenezwa, itarekebishwa na wananchi wake wataweza kuitumia kwa manufaa mapana ya kiuchumi na ya kijamii.