Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:- Je, nini mkakati wa Serikali kufanya utafiti kwa mazao ya kilimo na biashara ili kubaini uwepo wa changamoto katika msimu husika? (Makofi)

Supplementary Question 1

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Wizara yaliyoletwa na Mheshimiwa Waziri. Katika muktadha huo, basi kuna mazao ambayo sasa hivi imekuwa ni vigumu kuyauza, ikiwemo vanila inayolimwa Uru Kusini, pamoja na kahawa ambayo imekosa soko kutokana na deforestation. Mheshimiwa Naibu Waziri, unawaeleza nini wananchi wa Uru Kusini kuhusu jambo hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Bei ya kahawa imekuwa ikiyumba kila siku iitwayo siku. Nini hasa hatua ya Serikali kusaidia bei hiyo i-stabilize? (Makofi)

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa, Mama Shally, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu changamoto ya Sheria iliyopitishwa na EU ya Deforestation, hatua inayoichukua Serikali sasa hivi ni kwamba, Bodi ya Kahawa imeanza kufanya survey na kuanza utaratibu wa certification na kuwapatia wakulima na mashamba yao hati za ithibati ambazo zitasaidia uuzaji wa mazao ya kahawa katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili linafanywa kwa mazao ya kahawa, zao la cocoa, soya beans na mazao mengine. Kuna mazao sita ambayo kwa mujibu wa Sheria iliyopitishwa na Bunge la EU, ni lazima kama Taifa na dunia nzima, tuweze ku-meet hiyo standard na Serikali inachukua hatua hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumezuia kampuni binafsi kujichukulia shughuli hii. Jambo hili litafanywa na Serikali na tunaendelea kulifanya kwa sababu, bila ya hivyo wakulima wadogo hawataweza kulipia gharama za certification.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu changamoto ya zao la vanila, naomba tu nikuhakikishie kuwa sasa hivi, kama Serikali tunafanya mazungumzo ya mwisho na nchi kama India na delegation itakayoondoka na Mheshimiwa Rais ambayo Naibu Waziri atakuwemo, moja ya mkataba utakaosainiwa China ni pilipili pamoja na zao la vanila. Kwa hiyo, itatuondolea matatizo yanayotukabili katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu stabilization ya bei ya kahawa, kwanza nataka tu nitumie nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge na wakulima wa kahawa wote kwamba, hali ya kahawa na ongezeko la bei ya zao la kahawa ya Arabika hata Robusta katika msimu unaokuja inaonesha taswira itakuwa nzuri. Sasa hivi kama nchi tumeji-register katika platform kubwa ambazo tunapata price discovery wenyewe na kuweza ku-determine bei itakayotokea kwa wakulima. Kwa hiyo, pale panapotokea changamoto, tutaweza kukabiliana nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge lako Tukufu mlitupitishia Sheria (Agricultural Development Fund) mwaka 2023 na sasa tumeanza kuitengenezea vyanzo vya mapato. Mojawapo ya jukumu la Mfuko huu wa Maendeleo ya Kilimo itakuwa ni kutengeneza mfumo wa kutengeneza stabilization system ya kuweza kuwalinda wakulima huko mbele ambapo tutakuwa tunakabiliana na anguko la bei ya mazao ya wakulima. Tunaendelea kuujenga ushirika na tunaendelea kuujenga mfumo wa TMX ili tuweze kuwalinda wakulima na changamoto zinazowakabili. (Makofi)

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:- Je, nini mkakati wa Serikali kufanya utafiti kwa mazao ya kilimo na biashara ili kubaini uwepo wa changamoto katika msimu husika? (Makofi)

Supplementary Question 2

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kuiuliza Serikali, ni nini mkakati wao kuhakikisha kwamba mazao yetu kwa zile mbegu za asili yanaendelea kuimarishwa katika vyuo vya utafiti ili kuepuka adha wanayoipata sasa hivi kwa kutumia mbegu za kisasa ambazo mkulima anakuwa tegemezi, kila mwaka lazima anunue mbegu mpya badala ile ya zamani ambayo ilikuwa unaweza ukapanda hata misimu sita hadi saba? (Makofi)

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mabula, Mbunge wa Ilemela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama Serikali sasa hivi tumeshakusanya aina 330 za mbegu zetu za asili na tumeanza kuzifanyia mchakato wa kuzisafisha na kufanyia characterization. Vilevile tumefanya mabadiliko ya Kanuni ya Sheria ya Mbegu ili kuruhusu mbegu zetu za asili ziweze kuingia madukani kama certified seeds kama nyingine zilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini kwamba baada ya mwaka mmoja kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu mbegu zetu za asili zitakuwa madukani kama zinavyoonekana hybrid seed au OPV seed. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wataalamu wetu wa TARI tayari wameshakusanya mbegu zaidi ya 300 zinafanyiwa characterization, zinasafishwa na tutaanza kuzifanyia multiplication na kuzigonga muhuri wa TOSCI na kuziingiza madukani ili Mtanzania aweze kuzipata kama anavyohitaji mbegu nyingine zozote.

Name

Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:- Je, nini mkakati wa Serikali kufanya utafiti kwa mazao ya kilimo na biashara ili kubaini uwepo wa changamoto katika msimu husika? (Makofi)

Supplementary Question 3

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ili wakulima wa kahawa wanufaike na hasa Mkoa wa Kagera ni kuacha kuuza kahawa ghafi, waanze kuongeza thamani kwenye hizo kahawa. Nataka kujua mkakati wa Serikali kuzisaidia AMCOS kuweza ku-access machine ili waweze kukoboa wauze kahawa safi badala ya kuuza kahawa za maganda kama ilivyo sasa. (Makofi)

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikubaliane na Mheshimiwa Anatropia kwamba mwelekeo wa kuuza mazao ya kilimo katika raw form siyo mwelekeo sustainable kwa muda mrefu. Sasa hivi kama Wizara tumeanza kwanza kufanyia feasibilty study Kiwanda cha TANICA ambacho kitatugharimu fedha nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, study ipo hatua ya mwisho tukishirikiana na TADB na tutaanza kutenga fedha kwa ajili ya ku-revive kile kiwanda kiweze kufanya kazi kwa sababu ni mali ya ushirika na Serikali ndiyo ina ownership sasa hivi, kina hali mbaya. Lakini mchakato wa kufanya value addition ndiyo mwelekeo wa Serikali, ni hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba ni jambo ambalo lipo kwenye priority ya Serikali, linahitaji uwekezaji. Tutalipa kipaumbele kama inavyostahili ili wakulima waongeze thamani ya mazao yao na waweze kuondoka kwenye kuuza malighafi.

Name

Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:- Je, nini mkakati wa Serikali kufanya utafiti kwa mazao ya kilimo na biashara ili kubaini uwepo wa changamoto katika msimu husika? (Makofi)

Supplementary Question 4

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Hivi karibuni kumekuwa na sintofahamu kwenye suala zima la zao la mbaazi. Mheshimiwa Waziri, zao la mbaazi sasa hivi linauzwa shilingi 1,300 mpaka shilingi 1,400; lakini pili, hao wanunuzi wanaonunua hiyo mbaazi nao wamegoma kununua mbaazi kwa sababu wanasema hawana mahali pa kupeleka. Kwa hiyo, wakulima wetu wamebakia stranded, hawajui mbaazi wapeleke wapi, lakini na bei pia hawaelewi ni bei ya namna gani inanunuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nini kauli ya Serikali kuhusiana na suala zima la wanunuzi hao? Pili, bei elekezi ni ipi sasa? Serikali inamsaidiaje mkulima kujua bei elekezi ya zao la mbaazi hususan Wilaya ya Chemba na Kondoa?

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kunti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kauli ya kwamba hakuna pa kupeleka mbaazi siyo sahihi, ni kauli ambayo inasemwa na madalali ili kuweza kuiangusha bei ya mbaazi. Pili, ni kauli ambayo inasemwa kwa sababu watu hawataki kwenda kwenye Mfumo wa Stakabadhi ya Ghala na kupitia Vyama vya Msingi vya Ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali tumeweka mguu chini, mbaazi, ufuta na mazao tuliyoyatangaza kupitia COPRA ni lazima yauzwe kupitia stakabadhi ya ghala na lazima yauzwe kupitia Vyama vya Msingi vya Ushirika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu nikwambie leo hii sisi kama nchi tayari tumeji-register kupitia TMX kwenye Commodity Exchange Market za dunia. Bei ya mbaazi leo India ni dola 810, hatutarajii kwenye mnada bei ya mbaazi idondoke kati ya shilingi 1,700/=, au shilingi 1,800/= kupitia mnadani. Kwa hiyo, huo ndiyo mwelekeo wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaombe wakulima wa Kondoa, Chemba na maeneo hayo kuwa changamoto hii katika nchi yetu ipo maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni Chemba kwa maana ya Wilaya ya Kondoa yote. Suala la stakabadhi imekuwa ni changamoto...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, kwa kifupi please.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kusukuma ajenda ya Stakabadhi Ghalani kwa sababu kupitia TMX ndiyo inayotusaidia kupata price discovery. Kuna matatizo kwamba wanunuzi wa kati hawataki, lakini ni lazima twende huko. (Makofi)