Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Primary Question

MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza:- Je, lini TFS itawaruhusu Wananchi wa Busanda kufanya shughuli za kiuchumi katika hifadhi ya misitu iliyopo kati ya Geita na Katoro kwani haina miti?

Supplementary Question 1

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wananchi takribani 400,000 kutoka kata sita za Jimbo la Busanda wanaofanya shughuli za kiuchumi kwenye maeneo haya kwa sababu hayana miti, lakini Serikali imesema wazi kwamba inakwenda kuanza kupanda hekta 100 kati ya hekta 50,000. Kwa hiyo, hekta karibu 50,000 zinabaki hazijafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili. Kwa nini Serikali isiruhusu eneo fulani litumiwe na wananchi kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo kwa sababu hekta 50,000 zitakuwa zimebaki?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa nini wananchi wasigaiwe miche na TFS ili waanze kupanda miche hiyo wakati wakiendelea na shughuli za kiuchumi?

Name

Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge yote kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la msitu lililoharibika ni hekta 2,000 na siyo hekta 50,000 kama Mheshimiwa alivyokuwa anasema, lakini kwa sababu jambo analolishauri lipo katika taratibu zetu, pale ambapo tuna mpango wa kupanda miti huwa tunatoa ridhaa kwa wananchi kushiriki kwenye kupanda miti kwenye maeneo hayo, lakini vilevile kufanya shughuli za kilimo kwenye maeneo yale ambayo yamepandwa miti. Pale inapotokea kwamba miti hiyo imeshakua mikubwa, wananchi wanaacha kufanya shughuli hiyo ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili tunalichukua, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane ili tuweze kuweka mkakati utakaokuwa jumuishi kwa wananchi wote wanaohitaji kufanya shughuli hii na kuona mahitaji ya miche ya miti inayohitajika ili tuweze kujipanga na kuweza kutoa ridhaa na kuwasaidia.