Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Michael Mwita Kembaki
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Mjini
Primary Question
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani kuzuia uingizaji wa bidhaa bandia kutoka nje ya nchi ambazo ni hatari kwa watumiaji?
Supplementary Question 1
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali ambayo bado mimi sijaridhika nayo, ukienda katika maduka mengi ukitafuta bidhaa genuine huwezi kuipata. Je, maana yake ni kwamba Serikali haioni bidhaa hizi katika maduka yetu na katika soko ambalo lipo katika mitaa yetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kumekuwa na viwanda vingi bubu ambavyo vipo katika mitaa yetu, vingine vinatengeneza oil chafu ambayo tunatumia kuweka kwenye magari yetu. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba viwanda hivi ambavyo vinatengeneza bidhaa ambazo hazikidhi viwango vinadhibitiwa? (Makofi)
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Kembaki kwa kufuatilia masuala yanayohusiana na bidhaa bandia au bidhaa ambazo hazikidhi mahitaji katika soko letu. Ni kweli bado tuna changamoto ya bidhaa bandia, lakini siyo kweli pia kwamba hakuna bidhaa genuine katika maduka yetu kama ambavyo amesema Mheshimiwa Mbunge. Bidhaa zote zipo na niseme kuna watu ambao wanatumia nafasi hii moja kuingiza bidhaa hizi ikiwa ni sehemu ya kukwepa kodi na kufanya mambo mengine ambayo hayafai.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bidhaa genuine zipo lakini pia na bidhaa bandia zipo na ndiyo maana tuna Sheria ya Ushindani ili kuhakikisha tunafuatilia na kukagua kwenye maduka ili tubaini. Hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kwenye bidhaa ambazo ni bandia na tunashukuru kwamba wafanyabiashara na wazalishaji wanashirikiana na Serikali ili kutambua bidhaa ambazo siyo genuine katika maduka yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili, viwanda bubu ambavyo vinaingiza na kuzalisha bidhaa bandia tayari hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa, moja ikiwa ni kuwakamata na kuchukua hatua kali dhidi yao. Haya yamekuwepo siyo tu katika bidhaa alizozitaja Mheshimiwa Mbunge, lakini pia hata kwenye vinywaji.
Kwa hiyo, kuna wengine wanachukua vifungashio vya viwanda fulani halafu wanaweka bidhaa humo na kuanza kuuza mitaani. Kwa hiyo hatua zimekuwa zikichukuliwa ili kukabiliana na changamoto hii ya viwanda bubu, nakushukuru sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved