Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Esther Nicholus Matiko
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ESTHER N. MATIKO K.n.y. MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji uliokwama kwa muda mrefu katika Kijiji cha Mang’ola Juu Wilayani Karatu?
Supplementary Question 1
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, ila niseme tu nasikitishwa na majibu ya Mheshimiwa Waziri. Ni kweli kabisa kwamba mradi huu wa Mang’ola Juu umeanza ni takribani miaka mitatu sasa na umekuwa ukisuasua, umefikia 30% tu. Je, Serikali haioni kwamba mradi huu unakosa value for money? Serikali inachukua hatua gani za dharura kuhakikisha kwamba wananchi wa Mang’ola Juu wanapata maji kwa wakati kama ilivyokusudiwa hapo awali?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, tuna mradi wa maji wa Ziwa Victoria ambao unatoka kwa wananchi wa Rorya, Tarime Mjini na baadhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, lakini mradi huu nao utekelezaji wake umekuwa ukisuasua na ulitarajiwa kukamilika mwaka 2025, lakini mpaka sasa hivi ni 12.5% tu zimetekelezeka na mkandarasi ameondoka site kwa sababu ame-rise certificate ya 4.3 billion, hajalipwa mpaka sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujua, ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba inakuwa na uhalisia wa utekelezaji wa miradi hii ya maji ili wananchi wa Tarime wajue kwamba kufikia 2025 ni kweli mradi huu unaenda kutekelezeka?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ambavyo limeulizwa na Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi unapoanza, tunaanza na feasibility study na baada ya hapo tunafanya usanifu na baada ya hatua zote hizo ni utekelezaji wa mradi. Unapoanza kwenye upembuzi yakinifu, usanifu, hizo zote ni hatua, lakini sasa tunapokuja kwenye execution ya mradi ndipo sasa tunapoona kwamba zile asilimia zinapofikia tunaelewa kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa, nakiri kwamba mradi huu ulianza miaka mitatu iliyopita, lakini kuanza rasmi ujenzi wenyewe hauna muda mrefu kama ambavyo Mheshimiwa ameugusia. Ninachotaka kusema ni kwamba Serikali imejidhatiti kuhakikisha kwamba miradi hii, kwa sababu lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunaendelea na falsafa ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mama ndoo kichwani, tutahakikisha mradi huu wa Mang’ola Juu unakamilika kwa wakati na wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo linaenda sambamba na suala la mradi wa Ziwa Victoria kutokea kule Rorya. Ni kweli nakiri kabisa kwamba tulipata changamoto na mkandarasi hapa katikati, lakini tayari tuko kwenye mazungumzo naye ili kuhakikisha kwamba anarudi site na kuhakikisha kwamba mradi unaendelea wakati mahitaji yake na madai yake yanaendelea kufanyiwa kazi na Serikali, kwa sababu tunajua kabisa kwamba Tanzania hii tutaijenga sisi wote na wakandarasi ni Watanzania wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Name
Esther Edwin Maleko
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ESTHER N. MATIKO K.n.y. MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji uliokwama kwa muda mrefu katika Kijiji cha Mang’ola Juu Wilayani Karatu?
Supplementary Question 2
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Je, ni lini mradi unaoendelea katika Kata ya Mwika Kusini utakamilika? Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari tuongozane mguu kwa mguu kwenda kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa sababu wananchi hawa wanateseka sana kwa shida ya maji?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, niko tayari kuongozana mguu kwa mguu, nakushukuru sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved