Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Primary Question

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:- Je, Serikali imejipangaje kuwahusisha vijana waliomaliza mafunzo ya JKT waliopo katika vikosi na waliohitimu katika Mpango wa Block Farming?

Supplementary Question 1

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, naomba ufafanuzi zaidi kwenye jibu lako, hapo ulipoanzia; “Aidha, kwa wale waliokwishaanza wenyewe na kuwa na changamoto ya mikopo tunahimiza wawasiliane na Mfuko wa Pembejeo.” Sijaelewa connection yake na swali langu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kwa nini Serikali kupitia Wizara ya Kilimo isione umuhimu kwamba wale vijana wanaopata mafunzo ya BBT wawe wanafundishwa na wanakuwa attached kule walikotoka kwenye halmashauri zao ili waweze kueneza ule ujuzi kwenye halmashauri badala ya kuwabeba na kuwapeleka kwenye block farming?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jesca, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana kwa kufuatilia mpango huu wa kujenga kesho iliyobora kwa vijana katika sekta ya kilimo. Katika BBT kuna maeneo manne ambayo Serikali inayafanyia kazi. Moja, ni hayo ya block farming ambalo liliulizwa kwa maana ya mashamba makubwa; sehemu ya pili ya financing kwa maana ya mikopo kwa wale ambao wanakuwa wamepata mafunzo hayo; sehemu ya tatu ni ya ugani ambayo nayo pia tunaiangalia; na sehemu ya nne ni ya kuhakikisha maji yanapatikana kwenye mashamba hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuhusiana na ufafanu wa eneo la kwanza ni kwamba kulingana na swali lake kwamba tumefanya makubaliano na JKT, lakini kuna vijana wengine ambao walipita JKT hawatakuwa kwenye huu mpango. Kwa hiyo, tunasema wale ambao watakuwa wamepita BBT lakini hawapo kwenye huu mpango ambao tumekubaliana MOU na JKT maana yake na wao tunachukulia wameshapata ujuzi. Sasa kwa sababu kwenye mpango huu hawa watapata fedha kwa maana ya ukopeshwaji watakapokuwa wamepita kwenye block farming hizi, sasa wale ambao hawako kwenye utaratibu huu maana yake tunawashauri wapate financing kupitia Mfuko huu wa Pembejeo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na sehemu ya pili, kama nilivyosema ni kwamba tayari tunawaandaa vijana kulima kisasa kwenye mashamba haya ya block farming. Wengine ambao watapenda kwenda zaidi ni wale ambao watapata mafunzo ya ziada ya ugani na hawa tutawaelekeza warudi kwenye maeneo waliyotoka kwa wakulima. Pia, hata wale wengine ambao wanaweza kuwa hawajapata mafunzo haya mahususi ya ugani pia tunachukua wazo hili kwamba nao wakipata nafasi sasa badala ya kukaa kwenye mashamba haya ya block farms kubwa wanaweza wakarudi wakashirikiana na wakulima kule vijijini walikotoka ili kueneza ule ujuzi walioupata kuwasaidia wakulima wengine, nakushukuru sana. (Makofi)