Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Norah Waziri Mzeru

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NORAH W. MZERU aliuliza:- Je, lini Serikali itaajiri Walimu wa kutosha kutokana na ongezeko kubwa la Wanafunzi?

Supplementary Question 1

MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza. Pamoja na kazi nzuri ya Serikali katika kuendelea kuajiri walimu. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha mazingira ya kazi na motisha kwa walimu, hususan wale wanaoishi na kufanya kazi vijijini? Hili ni muhimu, ili kuzuia walimu wengi wanaokimbilia mijini na kusababisha upungufu wa walimu vijijini. Ahsante.

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, hoja ya Mheshimiwa Mbunge ni hoja ya msingi na Serikali inatambua umuhimu wa motisha kwa walimu, hasa wale wanaofanya kazi vijijini, ili waweze kufanya kazi kwa hamasa. Kwa hiyo, mkakati wa Serikali katika eneo hili kwanza ni kujenga nyumba za kuishi kwa walimu, ili kuboresha mazingira yao ya kazi wanapokuwa wanafanya kazi katika maeneo yao ya vijijini.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali imekwishajenga nyumba 253 ambazo zinabeba familia mbili. Kwa hiyo, hii ni sehemu ya mkakati wa kuboresha mazingira ya walimu wanaofanya kazi vijijini.

Mheshimiwa Spika, pili, Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba, walimu wanalipwa malimbikizo yao na stahiki zao kwa wakati. Katika Mwaka 2022/2023 Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 22.73 za madeni ya walimu yasiyokuwa ya mishahara. Kwa hiyo, hii ndiyo mikakati ambayo Serikali inaendelea kufanya, ili kuhakikisha walimu wanaofanya kazi vijijini wanafanya kazi kwa hamasa.