Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Yahya Ally Mhata
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Primary Question
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha uzalishaji wa zao la korosho katika Wilaya ya Nanyumbu?
Supplementary Question 1
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza; katika kuboresha zao la korosho ni pamoja na kutoa bei nzuri kwa wakulima wa korosho. Je, lini Serikali itatoa bei elekezi ya zao la korosho, hasa ukizingatia kwamba msimu wa korosho unaanza tarehe 01 Septemba, mwaka huu 2024?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili: Kwa kuwa, uzalishaji wa zao la korosho ndani ya Wilaya ya Nanyumbu umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka, na hivyo kusababisha Chama Kikuu cha Ushirika kushindwa kutekeleza majukumu yake ya msingi: Je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba wakati umefika Wilaya ya Nanyumbu ikaanzisha Chama chake Kikuu cha Ushirika, ili kuwa karibu zaidi na wananchi?
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka huu wa fedha 2024/2025, mfumo utakaotumika katika ununuzi wa korosho ni mfumo wa TMX, yaani soko la bidhaa kupitia TMX. Ukweli ni kwamba, safari hii hatutakuwa na bei elekezi isipokuwa tutakuwa na base price, yaani bei ya msingi ambayo itakuwa inajumuisha gharama zote ambazo mkulima alizitumia katika kuzalisha kilo moja ya korosho. Kwa hiyo, mnunuzi hatanunua chini ya hiyo base price kupitia mfumo wa TMX. Bei hiyo tutaitoa mwezi Septemba, 2024 kwa sababu, nimeshajadili na kuzungumza na Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho na amenihakikishia kwamba, atalifanya hilo mara moja.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuanzisha Chama cha Msingi cha Nanyumbu, maana yake inajiondoa katika Chama cha MAMCU. Sisi kama Wizara hatuna pingamizi na jambo hilo, isipokuwa Wilaya ya Nanyumbu wanapotaka kuanzisha chama hicho wafuate taratibu zote ikiwemo kuita Mkutano Mkuu wa Wanachama wote wajadiliane. Jukumu letu kama Wizara litakuwa ni kuwaongoza ili kufikia lengo ambalo wanalihitaji. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved