Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Primary Question

MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:- Je, kwa nini majengo ya zamani ya Halmashauri ya Bunda DC yasitumike kuwahudumia wananchi wa Jimbo la Bunda?

Supplementary Question 1

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imekiri kwamba haya majengo yaliyokuwa Halmashauri ya Bunda yako wazi na yamepangishwa na umiliki wa majengo hayo utakuwa umemalizika mwezi Desemba, 2024. Je, Serikali iko tayari kurudisha Halmashauri ya Bunda kwenye eneo hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wananchi wa Bunda takribani 175,000 wanasafiri umbali wa kutoka Jimbo la Bunda kwenda Halmashauri ya Bunda (TC) ni kilometa 50; kutoka Bunda (TC) kwenda Bunda (DC) ni kilometa 70; jumla kilometa 120, hivyo kwenda na kurudi ni 240. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwahurumia watu wa Bunda kuwarudisha Jimbo la Bunda au kuwapa halmashauri yao? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Getere kwa ufuatiliaji wa suala hilo, amefuatilia mara kadhaa, lakini nimwambie mambo mawili. Kwanza, Serikali ilitoa maelekezo ya Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kuwa na Makao Makuu ya Halmashauri katika maeneo ya kiutawala ya halmashauri husika. Hilo lilikuwa ni zoezi la Kitaifa na hivyo Halmashauri ya Bunda ililazimika kuhama kutoka Bunda Mji kwenda Bunda Vijijini. Hayo ni maelekezo ya Serikali na ni lazima yaendelee kutekelezwa ili kusogeza huduma kwa wananchi. Kwa hiyo Serikali haiko tayari kuwarudisha Halmashauri ya Bunda Vijijini kuja kufanya kazi ndani ya Bunda Mji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili kuhusiana na umbali, ni kweli kwamba wananchi wa Bunda Vijijini na hususani wanaotoka Jimbo la Bunda Vijijini wanasafiri umbali wa zaidi ya kilometa 120 kwenda Mwibara kwa ajili ya kupata huduma za halmashauri. Sasa naomba tulichukue jambo hili, kwa sababu lengo la Serikali ni kusogeza huduma kwa wananchi. Sisi na Mkoa wa Mara, Halmashauri na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutajadiliana tuone njia nzuri ya kutatua changamoto hiyo, ahsante. (Makofi)