Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Deus Clement Sangu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwela
Primary Question
MHE. DEUS C. SANGU K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:- Je, lini Serikali itamaliza changamoto ya umeme Wilayani Nkasi?
Supplementary Question 1
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mabadiliko ya bei, hasa katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Namanyele na Laela, ziliathiriwa ambapo kutoka shilingi 27,000 mpaka shilingi 320,000 kutokana na Sheria ya Mipango Miji, lakini kiuhalisia Sura ya Mamlaka ya Miji hii midogo ni ya vijiji. Je, Serikali mna mpango gani wa kushusha bei kurudi kuwa, shilingi 27,000 ili kuwapa nafuu Wananchi wa Mamlaka ya Miji hii kuunganisha umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme Mkoa wa Rukwa, hasa Jimbo la Kwela, speed yake ni ya kusuasua, hasa katika Kata ya Mnokola, Kilangawala na Milepa. Nataka kupata kauli ya Serikali, ni lini mtamsimamia mkandarasi huyu kikamilifu, ili aweze kutekeleza majukumu kwa sababu, tumelalamika mara nyingi hapa Bungeni? (Makofi)
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na maeneo ambayo wana-charge shilingi 320,000 badala ya shilingi 27,000 katika maeneo ya Namanyele na eneo lingine ambalo Mheshimiwa Mbunge amesema.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, tumefanya mapitio ya maeneo ambayo tuliona hayastahili kuwekewa kiasi cha shilingi 320,000 na tumeshauri, ili iweze kushuka mpaka shilingi 27,000. Katika maeneo haya tumeshapitia maeneo 1,500 na tumejiridhisha kwamba, inabidi yaende kwenye shilingi 27,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na maeneo haya mawili ambayo Mheshimiwa Mbunge amesema tutaenda kupitia kuona kama yapo katika yale maeneo ambayo tumesema, inabidi yatoke shilingi 320,000 mpaka shilingi 27,000. Kama yapo hapo tutaendelea na utekelezaji kwa kadiri muda unavyoenda na upatikanaji wa fedha, lakini kama hayapo, basi tutajiridhisha kuona kama maeneo haya yanatakiwa kushushwa mpaka shilingi 27,000 na baada ya hapo tutayaingiza katika mpango huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na haya maeneo ya Kwela, Mnokola, Kiwangawala na hilo lingine ambalo amesema Mheshimiwa Mbunge; kwa kweli, ni kweli huu Mradi wa Tanzania – Zambia Interconnector ulikuwa unasuasua kidogo kwenye baadhi ya maeneo. Mapema mwaka huu Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati walifanya ziara kwenye mradi huu na kukwamua yale matatizo ambayo yalikuwa yanasababisha mradi kutoenda kwa kasi ambayo sisi tumetarajia. Nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wameshafanyia kazi na tutaendelea kumsimamia mkandarasi, ili aweze kutekeleza vizuri mradi huu uweze kukamilika kwa wakati. Ahsante.
Name
Selemani Moshi Kakoso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Vijijini
Primary Question
MHE. DEUS C. SANGU K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:- Je, lini Serikali itamaliza changamoto ya umeme Wilayani Nkasi?
Supplementary Question 2
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza, naishukuru Serikali kwa kupeleka Miradi ya Umeme wa REA kwenye Wilaya ya Tanganyika. Kwenye Wilaya ya Tanganyika mmepeleka Umeme wa REA kwenye Kata ya Mwese ambao umewafikia wananchi. Kwa bahati mbaya sana zile taasisi muhimu kama soko, Parokia na eneo la Msikiti na shule ya sekondari na msingi hakujapelekwa umeme. Ni lini mtapeleka huduma hiyo iwafikie wananchi?
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Kakoso, Mbunge wa Tanganyika. Ni kweli katika maeneo mengi, ikiwemo hii Mwese, kuna baadhi ya taasisi hazijafikiwa, lakini tumeshatoa maelekezo kwa yale maeneo ambayo hayadizi mita 500, basi wafanyie kazi kuona taasisi ambazo zipo kwenye ukubwa wa sehemu ambapo umeme ulipo mpaka mita 500 yaweze kuunganishwa na umeme kwa sababu, wote tunafahamu umuhimu wa taasisi hizi katika mendeleo ya jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, katika Kata hii ya Mwese ambapo Mheshimiwa amesema maeneo ya parokia, msikiti, shule za msingi na sekondari tutafanyia kazi. Tutakwenda, ili kuweza kuona kama maeneo haya yapo kwenye ukubwa huo na kuweza kupatiwa umeme, lakini kama maeneo haya yapo mbali tutaangalia kuona kwenye mradi wa vitongoji kuona namna gani maeneo haya yanafikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, ni azma na nia yetu ya dhati kuhakikisha maeneo yenye taasisi zote za muhimu yanafikiwa na umeme kwa sababu, Serikali inawekeza fedha nyingi sana, hususan kwenye shule za msingi na sekondari. Na dhamira yetu ni kuhakikisha maeneo haya yenye taasisi zinazoleta huduma kwa jamii na zenyewe zinaweza kupata umeme, ili tuweze kuboresha zaidi mazingira ya kujifunza na kujifunzia kwenye shule za msingi na sekondari. Ahsante.
Name
Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba kusini
Primary Question
MHE. DEUS C. SANGU K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:- Je, lini Serikali itamaliza changamoto ya umeme Wilayani Nkasi?
Supplementary Question 3
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Utekelezaji wa Miradi ya REA katika Wilaya ya Muleba unasuasua. Serikali ina kauli gani kumuhimiza mkandarasi amalize ile kandarasi aliyopewa? (Makofi)
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na pia, nashukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Kikoyo. Nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kweli, ni mkakati wetu kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati. Namhakikishia nitafanya ziara katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge, ili kujionea na kuendelea kumsisitiza mkandarasi aweze kuongeza kasi hii ya kupeleka umeme kwenye vijiji ambavyo vimebakia, ili iweze kufanyika kwa haraka wananchi waweze kupata umeme. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved